Monday, June 06, 2011

ARE You Serious??!!!

Rozari ya wakatoliki

Tasbihi ya Waislamu

Hirizi ya wote hata wasio waamini

Na Victor Makinda
           Mimi si muumini wa dini za mapokeo. Nilishawahi kulieleza hili mara nyingi katika maandiko yangu hususani gazetini Rai katika ukurasa wangu  wa 15, Tafakuri ya Makinda ya kila Alhamisi. Mimi  ninaamini katika nguvu ifanyayo nguvu na  iletayo nguvu. Haijalishi chanzo cha nguvu hiyo. Hapa panahitaji maelezo marefu. Inatosha tu kusema kuwa imani ni kuamini, ni kukubali pasipo kuhoji uhalali na uhalisia wa kile ukiaminicho. Hii ndio sababu watu wanaamini uwepo wa Mungu aliye hai ilhali hawajawahi kumwona. Ni imani tu. Siwezi kukebehi wala kubeza imani za watu Nitakuwa wa mwisho kufanya hivyo. Lakini ninakerwa ninapomwona mtu, kikundi cha watu wanaasisi ama kutekeleza  mipango ya kibaguzi kwa misingi ya dini/imani za zao.

Ninamchukia sana kiongozi mdini na mpendelevu wa watu wa dini yake. Ninampenda sana kiongozi anayetoa fursa sawa kwa wote kwa kuzingatia uwezo/sifa na vigezo stahiki. Kwani silijui ni Taifa gain Duniani limeendelea kwa kuendekeza ubaguzi wa dini na upendelevu wa imani fulani.

 Ninapenda kuona umoja na mshikamano unaounganishwa na uzalendo na utaifa. Ninauchukia sana umoja unaounganishwa na imani ya dini fulani ambao msingi wa umoja huo ni kushikamana na kubagua wengine. Huwa natamani kufanya lolote kwa umoja wa aina hiyo. Ninampenda sana mtu anayehubiri dini kwa kusisitiza uwepo wa haki, amani na mshikamano kwa watu wote.Ninamchukia sana mtu yoyote anayehubiri dini katika misingi ya ubaguzi wa dini nyingine. Huyu huwa ninamuhisi kuwa akili zake zina walakini na uwezo wake wa kufikiri unatakiwa kuhofiwa. Ninamchukia/ninakichukia sana chama cha siasa  kilicho/kinachojijenga kwa misingi ya kidini. Ninakipenda sana chama kinachohubiri misingi ya Demokrasia na haki sawa kwa raia wote.

 Nina mengi ya kueleza. Tuna mifano mingi ya machafuko ya kidini na adha ziwapataz raia walio na wasio na dini katika maeneo yanayotawaliwa kwa misingi ya imani za kidini.   Nigeria ni moja kati ya mfano wa wazi unaotoa taswira ya ubaya wa ubaguzi wa dini katika uongozi wa Taifa. Huko machafuko ya kidini hayakomi kila kukicha hasa nyakati za uchaguzi. Sababu kubwa ni waumini wa dini moja kuona kuwa muumini/waumini wa dini nyingine hawafai kuongoza. Nchini Lebanon nako hali si shwari miaka nenda rudi. Ni machafuko ya kidini yasiyokoma. Sababu kubwa ni kugombania uongozi kwa misingi ya dini.

Hapa kwetu Tanzania kuna dini kuu mbili. Nazo ni Uislamu na Ukristo. Pia wapo wasio na dini ambao hawaamini hizi dini za Wazungu na Waarabu.Mimi ni mmoja wao. Kuna dalili za wazi za utengano wa kidini na ubaguzi. Tumeanza kuziona dalili hizo. Kuna kauli mbiu moja inayotumiwa na moja ya dini hizi inayosisitiza udugu baina ya waumini wa dini hiyo, inanikera sana. Kuna sababu gani kwa mtu wa dini A kukaririshwa kuwa ndugu yake ni mtu wa dini A. Hawa sasa wameathiriwa  na kauli mbiu hiyo.Inamaana wa dini B sio ndugu. Kauli mbiu hii inapaswa kufikiriwa upya na wahusika kwani inachochea ubaguzi na ubinafsi. Sitaki kuwachokoza watu hasa wenzangu wa upande huo kwani walishawahi kunishambulia sana na wangali wanafanya hivyo. Hawa waliniandalia kipindi maalumu katika moja ya vituo vya redio wanavyomiliki. Nataka kwa pamoja tutafakari nguvu ya Rozari, Tasbil na Hirizi kwa ajili ya ujezi wa Taifa lenye umoja na mshikamano.

 Kwa nini mvaa Rozari ahisi kuwa Rozari ina nguvu  na ubora zaidi kuzidi Hirizi? Kwa nini mshika tasbihi ahisi kuwa tasbihi ni bora zaidi ya Rozari na awaone kuwa wavaa Rozari hwastahili.? Vipi kuhusu mvaa Hirizi huyu naye kwa nini amuone na kumchukulia mvaa Rozari kuwa amapotea? Hawa wote ni wamoja. Wote wanafanana na wanaingia katika kundi moja la biniadamu. Ni dhana mbaya sana aliye upande mmoja wa imani kumbeza na kumbagua aliye upande wa pili. Hatari na athari tunaikaribia kuziona. Dalili na viashiria tayari tumeanza kuziona. Tusipofanya jitihada kubadilisha/kukbili hali hii hatupo mbali  kujutia matokeo. Hapo ndipo tutakapolia na kusaga meno.  
                                        Na liwe neno la leo.
 
   Victor Makinda
   Jumapili 5.June.2011
    Dar es Salaam.
     Simu 0716 45 89 13 email victormakinda@yahoo.com

No comments:

Post a Comment