KATIBU
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbroad Slaa
amesema Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya
Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, ni msaliti wa demokrasia nchini kwa
kuwa hana dhamira ya kutetea mageuzi ya kisiasa kwa maslahi binafsi.
Akihutubia
katika mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Luatala, Kata ya Sindano,
Jimbo la Lulindi mkoani Mtwara jana, Dk. Slaa alisema kuwa Maalim Seif
ni kiongozi asiyeeleweka, na ameshindwa kutumia chama chake cha CUF na
nafasi aliyonayo kutatua matatizo ya wananchi wanyonge, badala yake
amekifanya kipoteze heshima na mvuto ikiwa ni pamoja na kupoteza dhamira
ya kushika dola.
“Tulimuamini
Maalim na timu yake kuwa wangeweza kupambana kuisaidia mikoa ya kusini,
kwa maana wao washambulie huku na sisi maeneo mengine na kisha
tumuondoe adui. Lakini cha kusikitisha wenzetu wameungana na hao
tunaotaka kuwaondoa, na tunachoshuhudia huku sasa ni wananchi
kuaminishwa kuwa kuna vyama vya kidini vinafaya siasa,” alisema Dk.
Slaa.
Alisema
kutokana na usaliti wa kiongozi huyo, hatakuwa tayari kukaa nae meza
moja kwa ajili ya kuzungumzia siasa, hata kama ataombwa na wananchi, kwa
vile haaminiki na anaweza kumsaliti.
Alidai
kuwa, muungano baina ya Maalim Seif na chama chake na watawala,
umewafanya washindwe kupigia kelele uonevu unaofanywa na Serikali ya CCM
dhidi ya wakulima wa korosho katika mikoa ya Mtwara na Lindi, na badala
yake wabunge wa vyama hivyo (CUF na CCM) wakiungana kutetea vitu
visivyo vya msingi ikiwamo kudai posho katika vikao vya Bunge.
Dk.
Slaa alisema hakuwahi kuwa na tuhuma zozote za ufisadi, ndiyo maana
Serikali ya CCM inashindwa kumdhibiti kila mara anapoamua kuweka uozo
wao hadharani, badala yake imekuwa ikifanya kila mbinu kumsingizia mambo
yasiyo ya msingi, ambayo mwishowe wananchi hubaini hayana ukweli
wowote.
Mnyika ataka kauli ya JK kuhusu ushoga
Katika
hatua nyingine, CHADEMA kimemtaka Rais Jakaya Kikwete atoe tamko na
msimamo wa Tanzania kuhusu hatua ya Rais Barack Obama wa Marekani
kuidhinisha sheria ya ushoga nchini mwake.
Akihutubia
mkutano wa hadhara uliofanyika juzi kwenye Kata za Mnavira na Mchauru,
Jimbo la Lulindi, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika
alisema ukimya wa Rais Kikwete hauleti picha nzuri katika suala hilo
linalopingwa na dini zote.
Kauli
hiyo ya Mnyika ilifuatia swali aliloulizwa na Katibu wa Chama cha
Wananchi (CUF), Kijiji cha Rivango, Keneth Khamis aliyetaka kujua ukweli
kuhusu taarifa zilizowasilishwa kwao, zikieleza kuwa CHADEMA inaunga
mkono ushoga na usagaji, kutokana na kuwa na uhusiano na ushirikiano na
chama cha Conservatives cha Uingereza.
Alisema
hizo ni propaganda zilizopangwa na CCM ili CHADEMA kisikubalike katika
jamii, na kusema kauli iliyowahi kutolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi
wa CCM, Nape Nnauye ikiihusisha CHADEMA na kuunga mkono ushoga ni ya
unafiki.
Alisema
baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron kuukubali ushoga na
usagaji na kutaka iwe sehemu ya masharti kwa misaada inayotolewa na nchi
za Magharibi, CHADEMA ilipinga na kuweka wazi kwamba haiungi mkono
‘uchafu’ huo.
Mnyika
alisema kutokana na Rais Kikwete kwenda Marekani kwa lengo la kutafuta
misaada, kuna dalili ya kuwepo uwezekano wa taifa hilo kupenyeza ajenda
ya ushoga na ikakubaliwa na serikali kama ilivyotokea kwa Malawi.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment