Sunday, June 03, 2012

MAKAMANDA WA CDM

Dk Slaa: Maalim Seif msaliti


KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbroad Slaa amesema Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, ni msaliti wa demokrasia nchini kwa kuwa hana dhamira ya kutetea mageuzi ya kisiasa kwa maslahi binafsi.
Akihutubia katika mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Luatala, Kata ya Sindano, Jimbo la Lulindi mkoani Mtwara jana, Dk. Slaa alisema kuwa Maalim Seif ni  kiongozi asiyeeleweka, na ameshindwa kutumia chama chake cha CUF na nafasi aliyonayo kutatua matatizo ya wananchi wanyonge, badala yake amekifanya kipoteze heshima na mvuto ikiwa ni pamoja na kupoteza dhamira ya kushika dola.
“Tulimuamini Maalim na timu yake kuwa wangeweza kupambana kuisaidia mikoa ya kusini, kwa maana wao washambulie huku na sisi maeneo mengine na kisha tumuondoe adui. Lakini cha kusikitisha wenzetu wameungana na hao tunaotaka kuwaondoa, na tunachoshuhudia huku sasa ni wananchi kuaminishwa kuwa kuna vyama vya kidini vinafaya siasa,” alisema Dk. Slaa.
Alisema kutokana na usaliti wa kiongozi huyo, hatakuwa tayari kukaa nae meza moja kwa ajili ya kuzungumzia siasa, hata kama ataombwa na wananchi, kwa vile haaminiki na anaweza kumsaliti.
Alidai kuwa, muungano baina ya Maalim Seif na chama chake na watawala, umewafanya washindwe kupigia kelele uonevu unaofanywa na Serikali ya CCM dhidi ya wakulima wa korosho katika mikoa ya Mtwara na Lindi, na badala yake wabunge wa vyama hivyo (CUF na CCM) wakiungana kutetea vitu visivyo vya msingi ikiwamo kudai posho katika vikao vya Bunge.
Dk. Slaa alisema hakuwahi kuwa na tuhuma zozote za ufisadi, ndiyo maana Serikali ya CCM inashindwa kumdhibiti kila mara anapoamua kuweka uozo wao hadharani, badala yake imekuwa ikifanya kila mbinu kumsingizia mambo yasiyo ya msingi, ambayo mwishowe wananchi hubaini hayana ukweli wowote.
Mnyika ataka kauli ya JK kuhusu ushoga
Katika hatua nyingine, CHADEMA kimemtaka Rais Jakaya Kikwete atoe tamko na msimamo wa Tanzania kuhusu hatua ya Rais Barack Obama wa Marekani kuidhinisha sheria ya ushoga nchini mwake.
Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika juzi kwenye Kata za Mnavira na Mchauru, Jimbo la Lulindi, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika alisema ukimya wa Rais Kikwete hauleti picha nzuri katika suala hilo linalopingwa na dini zote.
Kauli hiyo ya Mnyika ilifuatia swali aliloulizwa na Katibu wa Chama cha Wananchi (CUF), Kijiji cha Rivango, Keneth Khamis aliyetaka kujua ukweli kuhusu taarifa zilizowasilishwa kwao, zikieleza kuwa CHADEMA inaunga mkono ushoga na usagaji, kutokana na kuwa na uhusiano na ushirikiano na chama cha Conservatives cha Uingereza.
Alisema hizo ni propaganda zilizopangwa na CCM ili CHADEMA kisikubalike katika jamii, na kusema kauli iliyowahi kutolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye ikiihusisha CHADEMA na kuunga mkono ushoga ni ya unafiki.
Alisema baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron kuukubali ushoga na usagaji na kutaka iwe sehemu ya masharti kwa misaada inayotolewa na nchi za Magharibi, CHADEMA ilipinga na kuweka wazi kwamba haiungi mkono ‘uchafu’ huo.
Mnyika alisema kutokana na Rais Kikwete kwenda Marekani kwa lengo la kutafuta misaada, kuna dalili ya kuwepo uwezekano wa taifa hilo kupenyeza ajenda ya ushoga na ikakubaliwa na serikali kama ilivyotokea kwa Malawi.

Tanzania Daima

Vodacom Yawashauri Wateja M-PESA Kutunza Namba Za Siri


KAMPUNI ya mawasiliano ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania imewatahadharisha  wateja wao wa huduma ya M-pesa kuwa  makini kulinda namba zao za siri zisifahamike  na watu wengine, kuepuka kuibiwa fedha zao.

Akizungunza na waandishi wa habari juzi ofisini kwake Mlimani city Jijini Dar es salaam, afisa mawasiliano na mahusiano Joseline Kamuhanda ameelezea madhara yatokanayo na kuvuja kwa namba za siri za mteja, hali inayosababisha wizi.

“Ukweli mteja akitoa namba  ya siri kwa wakala ili amsaidie kumtolea pesa katika akaunti yake ni hatari, kwa vile itategemea wakala huyo atakuwa na uadilifu wa kiasi gani, lakini pia hata kwa mtu wa karibu kumpa  kufahamu namba ya siri si jambo jema “ alisema Kamuhanda.

Akizungunzia kuboreshwa kwa mtandao huo  alisema M-pesa imezidi kuimarika baada ya kuondoa tatizo la ‘network’ kusumbua wakati Fulani, hali ambayo ilileta malalamiko kwa wateja.

“Tatizo la mtandao kusumbua katika zoezi utumaji pesa na upokeaji halipo baada ya wataalam kulifanyia kazi kikamilifu na kuliondoa” alisema Kamuhanda.

Akisisitiza kuhusiana na huduma za M-pesa afisa mkuu wa biashara Dylan Lennox amewaomba wateja kuwa na utamaduni wa kutuza namba za siri ikibidi kuzibadilisha kila baada ya muda, kuzuia hata ndugu wa karibu au rafiki kuikariri namba hiyo.

“Kuna watu wapelelezi wa mambo anakuzoea inafikia kujua namba ya siri ya akaunti yako, siku  unataka kutioa  fedha katika akaunti yako unaambiwa huna fedha za kutosha, badala yake unalaumu Vodacom wamekuibia kitu ambacho si kweli” alisema Lennox.

Alisema tatizo la mteja kuibiwa linahusiana na yeye mwenyewe kutoficha namba ya siri pengine kwa kutofahamu vyema namna ya njia za utoaji fedha kwa njia ya M-pesa, bila kujua  huyo aliyempa  namba ya siri  ameikalili na kutumia kumuibia.

Lennox anamalizia kwa kusema  kuwa Voda com imejipanga vizuri zaidi kwa ajili ya kuwapa watanzania na wateja wote kwa ujumla kuwapa huduma bora za kisasa ili kujiendeleza katika masuala ya kiuchumi na kijamii na kuwaomba watanzania waitumie vizuri huduma mpya ya wajanja
Na Zainul Mzinge

CHADEMA Waendelea Na Operesheni Okoa Kusini


Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe akiwahutubia wananchi wa mji wa Newala mkoani Mtwara, katika mkutano wa hadhara, leo. (Picha na Joseph Senga)
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe akiwauzia kadi wananchi waliojitokeza kujiunga na chama hicho, mara baada ya mkutano wake wa hadahara mjini Newala, mkoani Mtwara kwenye viwanja vya Mahakama.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe akiagana na wananchi wa kijiji cha Nanguruwe baada ya kuhutubia mkutano wa hadhara.

Waraka Wa Godbless Lema Kwa JK




IKULU ILIINGILIA KESI YA UCHAGUZI. – GODBLESS LEMA.

Ndugu Wananchi;


Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi na shukrani nyingi kwa ndugu zetu wa Arusha kwa kuwapokea vizuri na kuwakarimu vyema wageni wetu hao. Nawaomba waendelee na moyo huo mpaka watakapoondoka wote. Naomba kuwepo kwa mkutano huu kuwakumbushe umuhimu wa mji wenu kuwa tulivu. Miaka miwili iliyopita isingekuwa rahisi kwa watu au shirika kubwa la kimataifa kama Benki hii kuamua kufanya mkutano wake Arusha. Isitoshe hata sisi wenyewe tusingeshawishika kuomba au kukubali maombi ya namna hiyo. Lakini sasa imewezekana. Naomba kila mmoja wetu aweke azimio moyoni mwake la kuhakikisha kuwa hali ile haijirudii tena. Nyota ya Geneva ya Afrika lazima iendelee kuangaza. Yaliyopita si ndwele tugange yajayo
. ( J.K . KIKWETE.)

“Narudia tena , IKULU iliingilia kesi yangu ya Ubunge”.


Mh Rais nimekusikiliza kwa makini sana ila nakupa pole kwani bado unafikiri unaongea na Tanzania ya mwaka 1961 , umesema sasa Arusha ni shwari tofauti na miaka miwili iliyopita kwani sasa kuna amani na utulivu wa kutosha ndio maana hata mkutano wa AFDB umefanyika Arusha .


Mh Rais , najua IKULU iliingilia kesi yangu kama ilivyoonekana na ndio sababu hata Mkuu wa Mkoa wa Arusha wakati anaapisha Wakuu wa Wilaya alimpongeza Jaji kwa hukumu nzuri aliyowafurahisha wakati kesi hiyo iko mahakama ya Rufaa , lakini jambo moja la msingi ambalo huwezi kulitambua kwa sasa ni kuwa Haki na Ukweli haviwezi kushindwa na dhuluma, ubaya wala mamlaka , natambua wewe ni Rais na unayo mamalaka makubwa katika Taifa hili lakini vile vile nataka utambue kuwa huna mamlaka makubwa dhidi ya haki , utu na ukweli.


Mh Rais hakuna Amani Duniani inayozidi Haki na usawa ,utu na ukweli , haipo na wala haitakuwepo , ndio maana kila siku nasema ni
“Afadhali Vita Inayotafuta Haki na usawa kuliko Amani inayopumbaza na kudhalilisha utu wa Mwanadamu “ umefurahia sana mkutano uliokupa fursa ya kutoa maneno ya kebehi na kudhihirisha ila chafu iliyofanywa na Serikali yako na kujaribu kuhadaa Umma kama ilivyo kawaida ya Serikali yako na Chama chako , hata hivyo wakati huu kuna mambo ya msingi yakushughulikia zaidi ya kebehi na hadaa , Uchumi wa Nchi umeyumba, huduma za msingi za jamii zimepuuzwa, Mpasuko katika suala la Muungano na vururugu zinazoendelea Zanzibar , mfumuko wa bei hizi ni sababu chache ambazo haziwezi kuruhusu wakati huu kuwa wakati wa kebehi na mizaha isipokuwa kazi .

Mh Rais , Mama Theresa , Nelson Mandela , Martin Luther Jr na Malcom X hawakuwa Wabunge kupigania haki za Nchi yao na watu wao , sihitaji Ubunge kupigania ukweli, haki na utu , nahitaji dhamira safi , nia njema na huu utakuwa wajibu wangu mpaka nakwenda kaburini , nitakapomaliza mbio hizi najua nitapata fursa ya kutazama nyuma yangu nione nini nilifanya , ukweli nisingependa kuona vituo vya mafuta , magorofa , magari na viwanja vingi kila kona ya Nchi bali Haki ,Usawa na utu vikiwa kama nguzo ya imani ya watawala wetu watakaokuwepo, pengine sitaishi miaka mingi sana kama utachukizwa sana na waraka wangu huu kwani Polisi , Usalama wa Taifa na Jeshi la Wananchi wanakutii wewe , hata hivyo siogopi kufa kwani nisipokufa kesho , nitakufa siku moja ambayo siijui , napenda kuishi maisha marefu nimwone mke wa mtoto wangu kama itawezekana , lakini kuliko iwezekane kwa kuishi kwa hofu ni bora ishindakane kwa kuthamini haki , kwa hiyo kama utakuwa umekasirika sana , unaweza kufanya jambo lolote baya kwa kutumia mamlaka yako , niko tiyari sio kesho wala leo isipokuwa sasa hivi, najua IKULU imewazulumu watu wa Arusha Mbunge wao.


Mh Rais ninajua wazi njama zote na hasira hizi zinaweza kuwa zimetokana hasa na mkutano tuliokaa Osterbay Dar mimi na wewe kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 hata hivyo sikupuuza maongezi yetu isipokuwa nilichagua kufuata dhamira yangu na wito wangu wa utumishi wa kweli katika Jimbo langu na Nchi yangu.


Mh Rais nimekuelewa na Wananchi wamekuelewa kila mahali , wewe ni Rais unayo mamlaka makubwa na mimi ni mwananchi mamlaka yangu makubwa ni kwa mke wangu tu , sina Polisi wala Usalama wa Taifa lakini nitawaomba wanyonge wafunge na kusali tuone kama mamlaka yako inaweza kushindana na haki na ukweli .


Mh Rais
“Mtu anaweza kuzini kwa siri lakini hawezi kuugua ukimwi kwa siri” Serikali na Chama cha Mapinduzi kimepuuza watu na haki zao kwa muda mrefu , lakini wakati umefika ambapo hawatapuuzwa tena hata hivyo kwa kauli yako hii naamnini haiwezi kuwafundisha kazi majaji wa mahakama ya rufaa .

ONLY TIME WILL TELL”.


GODBLESS .J. LEMA.

Magazeti Leo Jumatatu