Ndugu zangu,
PICHA ya jeneza lililotelekezwa barabarani imeongea zaidi ya maneno milioni moja. Kwa Watanzania, imetutia simanzi, imetutoa machozi. Ndani ya jeneza hilo pichani kuna mwili wa marehemu Emmanuel Magige iliyotelekezwa kijijini Nyakunguru, Tarime. Emmanuel Magige hakuwa jambazi. Ni Mtanzania mwenzetu mwanakijiji wa kawaida. Aliyetelekezwa si Magige tu, kuna maiti nyingine tatu.
Mauaji ya Nyamonngo yanatukumbusha Arusha, yanatukumbusha Mbarali. Yanatutia hofu mpya pia. Hatujui kesho yatafanyika wapi.Kupunguza aibu hii ni kwa wote waliohusika na mauaji haya kuchukuliwa hatua za kisheria.
Jeneza la Emmanuel Magige lililotelekezwa barabarani ni kielelezo cha mahali tulipofikia. Kuna chuki inajengeka. Na katika tofauti zetu hizi za kiitikadi tusifike mahali tukashindwa kuongea kama Watanzania. Tusifike mahali tukachochea machafuko makubwa ya kijamii. Wanasiasa wana jukumu la kutanguliza busara katika kila maamuzi wayafanyao.
Na tuyalaani vikali mauaji ya Nyamongo. Tusipoyalaani nasi tutalaaniwa. Na Mungu huyu anatupenda Watanzania, kuna tunachoonyeshwa. Na tuzisome kwa makini alama hizi za nyakati. Na Miungu yetu, mizimu ya mababu zetu, inatupenda pia. Walikolala mababu zetu, nao wanaturajia tulaani kitendo hiki, maana, hata katika mila na desturi zetu, Waafrika hatutelekezi maiti zetu. Tunazizika.
Ndio, kwa jadi yetu, Waafrika tunahesabu wafu wetu, tunawatambua kwa majina, tunawaombea kwa imani zetu. Ndio, tunawazika wafu wetu. Kwa heshima zote.
Kwa desturi, Watanzania hatupendi kuwa katika hali ya kudharauliwa na kutothaminiwa kwa utu wetu tukiwa hai. Na kamwe, tusikubali Watanzania wenzetu wasithaminiwe wakiwa katika hali ya umauti. Na hilo ni Neno la Leo.
Temba DB
© MMXI
No comments:
Post a Comment