Thursday, May 26, 2011

LISSU na wenzake marufuku Nyamongo.

Mbunge wa Singida Mashariki na Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, Tundu Lissu akionyesha shati lake alilodai kuchaniwa na polisi baada ya kumpa kichapo akiwa nje ya Mahakama ya Wilaya ya Tarime, Mkoani Mara baada ya kupata dhamana jana. Picha na Anthony Mayunga




MBUNGE wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, na wenzake saba ambao juzi walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime na kusomewa mashtaka matatu ya kuingia eneo la hospitali bila kibali, kufanya mkutano na kuzuia watu kufanya kazi, wamepata dhamana lakini wamezuiwa kutembelea maeneo ya Nyamongo hadi kesi inayowakabili itakapokwisha.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya hiyo, Yusto Roboroga alitoa uamuzi huo akisema ni kwa mujibu wa kifungu cha Sheria Namba 148 cha Makosa ya Jinai, kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2002, ambacho kinatoa haki kwa watuhumiwa kupata dhamana. Alitoa uamuzi huo baada ya kupitia pingamizi lililowekwa na upande wa mashtaka kutaka wasipewe dhamana. Hata hivyo, alisema: “Washtakiwa wanazuiwa kutembelea maeneo ya Nyamongo mpaka kesi hiyo itakapokuwa imekwisha."

Hakimu huyo alisema kwa kuwa washtakiwa hao ni viongozi wakubwa wa chama walizuiwa ili kupunguza shinikizo la wanachama kutokana na tukio lililojitokeza, lakini kwa kuwa mazishi yameshafanyika, alisema wanaweza kudhaminiwa kama watakidhi masharti.
Hakimu Ruboroga alitaja masharti  ya dhamana hiyo kuwa ni kusaini mkataba wa dhamana wa Sh5 milioni kwa wadhamini wawili wanaoaminika.

Kwa wasio wakazi wa Tarime, alisema watatakiwa kupeleka mahakamani hati za mali isiyohamishika. Washtakiwa wote walikidhi masharti na kuachiwa kwa dhamana hadi Juni 26, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.

Juzi, Lissu na wenzake, Waitara Mwita Mwikwabe, Stanslaus Nyembea, Anderson Deogratias Chacha, Andrew Andalu Nyandu, Mwita Marwa Maswi, Bashiri Abdalllah Selemani na Ibrahimu Juma Kimu walifikishwa mbele ya mahakama hiyo na kusomewa mashtaka hayo matatu na Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Casmir Kiria ambaye alisema, waliyatenda Mei 23, majira ya saa nne usiku. Wote walikana mashtaka hayo.

Maiti wazikwa, wananchi wataka kurejesha majeneza polisi
Hatimaye maiti wote waliokuwa wametelekezwa barabarani wamezikwa na ndugu zao huku baadhi ya familia zikikataa kuwazika kwa majeneza ya polisi na kutumia yale yaliyokuwa yameandaliwa huku wengine wakipanga kuyarudisha kwa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Tarime, Constantine Massawe.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kewanja, Om’tima Tanzania alisema kuwa mmoja wa marehemu hao, Chacha Ngoka alizikwa na jamii. Hata hivyo, alisema polisi waliweka mwili wake ndani ya jeneza bila kuweka sanda hali ambayo iliwalazimu kumweka ndani ya jeneza lao na kumvika sanda. Hilo lilifanyika pia katika eneo la Nyakunguru alikozikwa marehemu Emmanuel Magige.

Katika Kijiji cha Bonchugu, Serengeti, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho, Mwikwabe Makena alidai kwamba walilazimika kuzika mwili wa marehemu Chawali Bhoke uliotelekezwa na polisi.
Alidai kwamba kabla ya kuutelekeza, walifyatua mabomu ya machozi na risasi hewani baada ya wananchi waliokuwa wamebeba pinde, mishale, mikuki na mapanga kujaribu kuzuia gari la polisi. Alisema walilazimika kuzika bila kuwapo kwa ndugu wa marehemu waliokuwa wameachwa Tarime.Hata hivyo, Kamanda Massawe na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Robert Boaz hakuwa tayari kuzungumzia madai hayo.

Wataka RC, DC wawajibishwe
Baadhi ya wananchi wamemtaka Rais Jakaya Kikwete kumwajibisha Mkuu wa Mkoa wa Mara, Enos Mfuru, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewelle na Kamanda Massawe kwa madai ya kushindwa kudhibiti uvunjifu wa amani.

Walisema viongozi hao wamekuwa wakijaribu kuficha ukweli wa kilichotokea katika mauaji hayo ya watu watano na kujeruhi wengine 10 na kusababisha kuvunjika kwa amani.

Mmoja wa wananchi hao, Marwa Sasi alisema kitendo cha polisi kufanya mauaji hayo na kuchukua maiti hospitali na kuzitelekeza njiani hakistahili kuachwa kipite hivihivi bila hatua kali za kinidhamu kuchukuliwa.
“Ukweli ni kwamba vijana wameuawa na kujeruhiwa. Tatizo ni nini litafutwe, si kudanganya umma mara walikuwa 800, 1,000 au 1,500, majambazi, wavamizi, walikuwa na silaha mbona tunaona majeruhi na maiti hatuoni askari waliojeruhiwa?”

Bavicha lakusudia kuandamana
Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) Mkoa wa Dar es Salaam limesema liko tayari kuandamana hadi magerezani kudai haki itendeke baada ya kutokea kwa mauaji katika tukio la uvamizi wa Mgodi wa Nyamongo.Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu wa Chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kilewo alisema kitendo hicho ni kinyume cha haki za binadamu. “Kitendo kilichofanywa na polisi cha kuwaua raia ni cha kulaaniwa na kupigwa vita ili kisijirudie tena kwa kuwa vitendo hivyo vinafanywa kwa maslahi ya wachache,” alisema.

Kilewo alisema kuwa chama hicho kitahakikisha haki inatendeka na kusisitiza kwamba kipo nyuma ya wananchi ambao ndugu zao wamefariki kutokana na tukio hilo... “Tutahakikisha kuwa Mtanzania anaheshimiwa katika taifa lake. Mauaji kama hayo yalitokea Arusha, sasa wameua tena Tarime... Hatuwezi kuvumilia kamwe.”

Wana Kawe nao wazungumzia mauaji Tarime
Kundi la watu waliodai kuwa wanawawakilisha wakazi wa Jimbo la Kawe wamewataka Mawaziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Nishati na Madini, kujiuzulu kwa kushindwa kuzuia mauaji ya wananchi yanayotokea mara kwa mara kwenye migodi nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kiongozi wa kundi hilo, Powell Mfinanga alisema kutokana na matukio ambayo yanahusisha wananchi wasio kuwa na hatia, umefika wakati wa viongozi hao kuwajibika.

“Inaonyesha kabisa wizara hizi zimeshindwa kufanya kazi ipasavyo kutokana na kuibuka kwa migogoro ya mara kwa mara kati ya wawekezaji wa madini na wananchi hali inayosababisha raia kupoteza maisha yao,” alisema Mfinanga. Alidai kwamba mpaka sasa zaidi ya watu 70 wamepoteza maisha kutokana na kuibuka kwa migogoro kati ya wawekezaji na wananchi wa maeneo ya machimbo ya madini.

Mfinanga ambaye alikuwa na zaidi ya wenzake 20 kwenye mkutano huo na waandishi wa habari uliofanyika Kawe, alisema wametoa msimamo huo kutokana na tukio la hivi karibuni la polisi kuwapiga risasi na kuwaua watu watano kwenye Mgodi wa North Mara, wiki iliyopita.

Aliitaka serikali ifanye uchunguzi huru na wa kina ili kujua chanzo na kuweka mkakati madhubuti utakaozuia mauaji hayo yasitokee tene.“Tusiishie kuwakamata watu wanaotuhumiwa kuhusika na tukio hilo. Ila kitu kinachotakiwa ni kufanya uchunguzi wa kina ili kujua nini chanzo cha mauaji hayo,” alisema Mfinanga.

(Chanzo- Mwananchi)

No comments:

Post a Comment