Tuesday, October 23, 2012

KUTOKA CHADEMA BLOG LEO

Uamuzi wa pingamizi la kesi ya Ubunge ya Godbless Lema ni Jumatatu

Aliyekuwa Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema (katikati) akiwa na Mawakili, Alute Mughway (kushoto) aliyesimamia kesi iliyomvua Ubunge na Mbunge wa Singida Mashariki ambaye pia ni wakili katika kesi ya kupinga kuvuliwa Ubunge wake, Tundu Lissu, katika msiba wao baba yao Alute na Lissu aliyefariki hivi kaibuni jijini Dar es salaam na kisha kuzikwa nyumbani kwao Singida. (picha ya Septemba 2012 via MjengwaBlog.com)
Uamuzi wa pingamizi zilizowekwa na mawakili wa pande zote mbili katika kesi ya uchaguzi Jimbo la Arusha Mjini dhidi ya aliyekuwa Mbunge wa CHADEMA, Godbless Lema utatolewa Jumatatu ijayo.

Awali wa upande wa majibu rufani katika kesi iliyomng’oa madarakani Lema, Alute Mughwai ambaye ni Wakili wa wanachama watatu wa CCM, aliiomba Mahakama ya Rufaa kutupilia mbali rufaa hiyo iliyowasilishwa kwao kwa kuwa ni batili na ina makosa mengi ya kisheria.

Habari za uhakika kutoka katika vyanzo vya habari ndani ya mahakama na kuthibitishwa na mmoja wa wanachama hao waliofungua kesi hiyo katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kupinga Lema kuwa mshindi katika Jimbo la Arusha, Mussa Mkanga vilisema kuwa pingamizi hizo zitatolewa uamuzi siku hiyo.

Mkanga alipoulizwa kama ana taarifa ya kusomwa kwa pingamizi hizo, siku hiyo alikiri kupewa taarifa na mahakama na kueleza kuwa siku hiyo watakwenda kusikiliza uamuzi wa pingamizi zao.

“Mimi na wenzangu kama walalamikaji tumeshapewa taarifa na mahakama juu ya siku na tarehe ya kusomwa pingamizi hizo na tuko tayari kwa hilo,” alisema Mkanga.

Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, George Hubert hakupatikana kuelezea taarifa hiyo baada ya simu yake ya mkononi kutopatikana, lakini habari za kimahakama zilithibitisha tarehe hiyo ya uamuzi.

Katika hoja zake za kutaka kesi hiyo itupiliwe mbali, Mughwai aliwaeleza majaji watatu wakiongozwa na Jaji Mkuu Othmani Chande kuwa kesi hiyo kuwa ni batili kwa kuwa imekosa vitu muhimu vya kisheria, ikiwamo tarehe ya rufaa hiyo kuandaliwa, kulalamikia kipengele ambacho hakijamtoa Lema madarakani pamoja na kutokuwa na muhuri wa Mahakama Kuu iliyoidhinisha rufaa hiyo.

Mughwai alisema katika nakala ya hati ya kukazia hukumu iliyowasilishwa mahakamani hapo, haina tarehe ya kuandaliwa kwake hali inayotia wasiwasi iwapo itakuwa imeandaliwa ndani ya kipindi kinachotakiwa kisheria cha siku 60 tangu kutolewa kwa hukumu au la.

Alidai mbali na nakala hiyo kukosa tarehe ya kuandaliwa kwake, pia haikuwa na muhuri wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kuthibitisha kuwa ni kweli imetolewa na mahakama hiyo kwa kuwa nakala hiyo ilikuwa na saini tu ya Jaji Gabriel Rwakibarila ambayo haithibitishi uhalali wake.

Naye Wakili wa waomba rufaa, Method Kimomogoro akijibu hoja hizo, alikiri kuwa ni kweli nakala hiyo ina upungufu na ni makosa ya kibinadamu ambayo hata hivyo hayana athari katika kesi ya msingi hivyo aliwaomba majaji kutupilia mbali pingamizi hizo.

Aidha, Wakili wa Serikali, Timon Vitalis aliunga mkono hoja zilizotolewa na Wakili Kimomogoro huku akidai  suala hilo la upungufu, lawama hazipaswi kuelekezwa kwa waomba rufani wala mawakili, bali zinapaswa kuelekezwa kwa mahakama ambayo ndiyo iliyoandaa hati hiyo.

Chanzo: http://www.wavuti.com/

Chadema kuchukua kata jimbo la Januari Makamba

Ni ukweli usiopingika kwamba Mkoa wa Tanga ni ngome ngumu kwa CDM lakini ukweli huu unakwenda kugeuka kuwa uongo.Kadri siku zinavyozidi kwenda ni dhahiri kwamba upepo wa mabadiliko unazidi kushika kasi na ukweli huu utaanza kudhihirika kwenye uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Tamota Jimbo la Bumbuli.

Nimepata fursa ya kuzunguka jimbo la Bumbuli, jimbo la Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia ndugu January Makamba na kujifunza mambo mengi tofauti na unavyoweza kumsikia na kumsoma kwenye magazeti, he deserve to be called Media Boy kwasababu hakubaliliki kwa namna ambavyo watu wengi wanaweza kufikiri zaidi ya kujenga jimbo kwenye magazeti na mitandao ya kijamii. Ukweli ni kwamba ni mwepesi mno silaha kubwa anayotumia ni nguvu ya fedha basi.

Kata ya Tamota ni moja kati ya kata 29 (moja ya kata mbili kwa Mkoa wa Tanga) nchi nzima ambapo kutakuwa na uchaguzi mdogo wa udiwani, kwa hali halisi ya kisiasa ilivyo ni dhahiri kwamba CHADEMA inakwenda kushinda na kuhesabu kata ya kwanza mkoa wa Tanga. Ni ukweli uliowazi kwamba ushindi wa kata hii utakuwa na maana kubwa kwa chama na hasa katika kueneza fikra za mabadiliko mkoa wa Tanga. Ni STAMINA Amir Sheshe anayetegemewa kutangazwa kuwa diwani wa kwanza wa CDM mkoa wa Tanga mnamo tarehe 28/10/2012.

Habari na Mbelwa Germano.

MAKAMANDA WA M4C (MAGOMA Jr MAGOMA-MWENYE KOMBATI YA KAKI, HENRY KILEWO-MWENYE KOMBATI NYEUSI, KAMANDA LEMA, M/KITI TANGA NA DIWANI MTARAJIWA KATA YA TAMOTA STAMINA- (MWENYE SUTI) WAKIWE KWENYE HARAKATI ZA KUSAMBARATISHA NGOME YA JANUARY MA KAMBA KATIKA KAMPENI ZA UCHAGUZI MDOGO KATA YA TAMOTA, ILI KUFIKA KATA YA TAMOTA TULIPITA BARABARA YA VUMBI UMBALI WA KM 85 KUTOKA SONI (LUSHOTO), KISHA TUKATEMBEA KWA MIGUU KM 6 ILI KUFIKA KIJIJINI ALIKOZALIWA MZEE YUSUPH MAKAMBA

Mnyika: Watendaji hawaelezi ukweli tatizo la umeme


WAZIRI Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, ameeleza kusikitishwa na kauli za viongozi na watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kuhusu hali ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini sanjari na uboreshaji wa utendaji TANESCO.
Amesema kauli hizo zinatoa matumaini potofu kwa wananchi na kuwasihi kuzipokea kwa tahadhari kwa kuwa hazielezi ukweli kuhusu tatizo la umeme nchini.
Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Ubungo, alitoa kauli hiyo jana katika taarifa yake kwa vyombo vya habari na kusema kulingana na nyaraka alizonazo za ndani ya wizara hiyo na TANESCO kuanzia Septemba hadi Oktoba mwaka huu, hali ya uzalishaji na usafirishaji na usambazaji wa umeme imekuwa tete kwa sababu mbalimbali ikiwemo upungufu wa upatikanaji wa mafuta na gesi asili kwa ajili ya uendeshaji wa mitambo ya kufua umeme na kasi ndogo ya uwekezaji kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa kudumu.
Mnyika pia alisema amemwandikia barua Spika wa Bunge, Anne Makinda, ili Wizara ya Nishati na Madini iwajibike kueleza hali halisi katika mikutano ya kamati za Bunge inayoendelea.
“Katika barua hiyo nimependekeza pamoja na mambo mengine suala la kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme na utekelezaji wa mpango wa uboreshaji wa utendaji wa TANESCO lishughulikiwe na kamati nyingine kwa haraka kwa kuzingatia maelezo na maelekezo ya Spika aliyoyatoa bungeni wakati wa kuahirisha mkutano wa nane wa Bunge,” alisema.
Aidha alisema mapitio ya utekelezaji wa mpango wa uboreshaji wa utendaji wa shirika hilo yahusishe kamati ya kudumu ya Bunge na itakayoeleza hatua iliyofikiwa katika uchunguzi wa tuhuma za ufisadi kwa kuzingatia kuwa siku 60 za uchunguzi zimepita.

Tanzania Daima

Sunday, October 21, 2012

CHADEMA yaeleza chanzo cha vurugu za Waislamu Dar



IMEELEZWA kuwa vurugu za kikundi cha Waislamu zilizotokea Mbagala hivi karibuni ni matokeo ya muda mrefu ya serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete kupuuzia kushughulikia matatizo yao.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mabere Marando na Profesa Abdallah Safari, wakati wakizungumza na waandishi wa habari juu ya msimamo wa chama hicho dhidi ya vurugu za kidini zilizotikisa Jiji la Dar es Salaam wiki hii.
Marando alisema kuwakamata viongozi wa Kiislamu pasipo kushughulikia matatizo yao si njia sahihi kwani kuna hatari ya kuzalisha Waislamu wengi wenye msimamo mkali dhidi ya serikali na kuifanya nchi kutotawalika.
“Kabla ya uhuru Waislamu walikuwa na taasisi zao serikali ya TANU, kwa ajili ya kulinda masilahi yake ikavifutilia mbali na kuamua kuwawekea Waislamu Bakwata na kutunga sheria za kuongoza, nataka mtambue matatizo ya Waislamu wote hayasimamiwi na Bakwata, waitwe Waislamu na waulizwe shida zao,” alisema Marando.
Aliongeza kuwa kabla ya uhuru Waislamu walipambana kwa kuamini walikuwa wakinyanyaswa na kwamba baada ya uhuru hawakuona mabadiliko yoyote, hivyo wanalazimika kujitafutia uhuru mwingine mbali na ule wa kutoka katika mikono ya wakoloni.
Alisema serikali isisubiri vifo vitokee ndiyo ione umuhimu wa kushughulikia matatizo hayo na badala yake ijipe muda wa kukaa na makundi yote kutafuta muafaka.
“Siamini kama kuna tatizo baina ya Waislamu na Wakristo bali mfumo wa serikali unawalazimisha Waislamu kuamini hivyo kwa kuwa wametengwa, hawasikilizwi hawathaminiwi na sasa wako kama yatima kwanini?” alihoji Marando.
Akizungumzia utekwaji wa watu unaoendelea nchini, Marando alisema serikali haiwezi kukwepa lawama hizo na kwamba matamshi ya viongozi wa Ikulu kuwa hawamfahamu Ramadhani Ighondu ni hadaa kwa Watanzania.
“Sheikh Farid alipotea katika mazingira ya ajabu na hili ni jukumu la serikali kujua hatima ya raia wake lakini leo tunaona vyombo vya ulinzi vikisema havihusiki wala havina habari na kupotea kwake, haya ni majibu kama yale yale yaliyotolewa kwa Dk. Ulimboka,” aliongeza Marando.
Kwa upande wake Profesa Safari alizungumzia kitendo cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania kuingilia kati kutuliza ghasia inaonesha kuwa serikali imeshindwa kuongoza nchi kwa kufuata sheria.
“Jeshi la Wananchi limefuata nini mtaani? Kuna tishio gani la amani inayowalazimisha wao kuingia mtaani? Kwa kuwa tunafahamu suala la kutangaza hali ya hatari na jeshi kuingia mtaani lazima liwe na baraka ya Bunge,” alisema Safari.
Aliongeza kuwa mara nyingi serikali imeshauriwa kutatua migogoro baina ya Waislamu na serikali, lakini ushauri huo umekuwa ukipuuzwa.

Tanzania Daima

Saturday, October 20, 2012

Mfadhili wa CCM ajiunga na CHADEMA



Chadema jana ilifanya Mkutano wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma kwenye mkutano wa hadhara wa kumnadi mgombea udiwani kata ya Mpwapwa kamanda Baharia.

Mkutano huo ulikuwa na umati mkubwa sana watu. Shangwe, hoihoi na nderemo vililipuka pale mfadhili mkubwa wa CCM mkoani Dodoma ndugu Shelali alipoamua kujivua gamba na kujiunga na CHADEMA. Alipopewa nafasi ya kusema chochote kwa umati ule ndugu Shelali alisema amekuwa mfadhili wa CCM tangu mwaka 1983.

Katika kuthibitisha hilo alikuja na nakala za barua za kuombwa fedha na mzee Malechela pamoja na tuzo nyingi za heshima kutoka CCM. Mzee Shelali alisema ameamua mwenyewe kujiunga na CHADEMA kwani ndicho chama pekee kinachoonyesha nia ya dhati ya kuikomboa Tanzania na kuwaomba wananchi wa Mpwapwa kujiunga na Chadema.

Katika mkutano huo ngugu Shelali alijitolea kuwanunulia kadi za CHADEMA wananchi wote watakaotaka kujiunga na CHADEMA wilayani mpwapwa. Baada ya mkutano huo wananchi na viongozi wa CHADEMA walielekea nyumbani kwa shelali kushusha bendera ya CCM na kupandisha ya CHADEMA ambapo mzee Shelali alijitolea kuipa CHADEMA ofisi.

Katika mkutano huo wananchi wa Mpwapwa walichanga zaidi ya sh. laki tano kwa ajili ya kusaidia kampeni. 

Kilichonifurahisha ni kitendo cha wananchi kuingia barabarani licha ya kuzuiwa na polisi waliojaribu kuzima maandamano yao.

Mkutano huo ulihutubiwa na Benson Kigaila, Diwani Ali Issa Biringi na Kamanda Nicholaus Ngowi.

Tuesday, October 16, 2012

Mnyika kuwasha moto zuio la fao la kujitoa mifuko ya kijamii


MBUNGE wa Ubungo (Chadema) John Mnyika amewasilisha kwenye ofisi za Bunge kusudio la muswada binafsi wa kubadili sheria moja ya vipengele vinavyosimamia kanuni za mafao kwa Taasisi ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kuhusu kusimamishwa kwa fao la kujitoa.
Mnyika aliwasilisha kusudio hilo kwa Katibu wa Bunge jijini Dar es Salaam jana akisema amefanya hivyo baada ya kubaini Serikali iko usingizini licha ya kuahidi kufanya marekebisho ya sheria hiyo.
Mbunge huyo alieleza hayo jana kupitia taarifa yake kwa gazeti hili akisema anatarajia kuwasilisha katika Bunge lijalo muswada binafsi wa sheria ya Marekebisho ya sheria za hifadhi ya jamii kwa hati ya dharura akizingatia kanuni ya 81 ya Kanuni za Kudumu za Bunge toleo la 2007.

“Lengo la Muswada huu ni kufanya marekebisho yenye kuboresha mfumo wa utoaji wa mafao nchini ikiwemo kuwezesha kutolewa kwa fao la kujitoa na mafao mengine muhimu ambayo hayatolewi katika utaratibu wa sasa wa mifuko mbalimbali ya hifadhi ya jamii,” alisema Mnyika.
Mnyika alisema amefikia uamuzi huo kwa kuwa mpaka sasa zimebaki siku chache Mkutano wa Tisa wa Bunge kuanza wakati Serikali imekaa kimya licha ya kuahidi kuwa itapeleka marekebisho ya Sheria ya Hifadhi ya Jamii Bungeni.

“Mpaka sasa Serikali haijaitisha mkutano na wafanyakazi pamoja na wadau wa jamii kupokea mapendekezo, hali ambayo inaashiria upo uwezekano muswada huo usiwasilishwe kwa wakati,” alisema Mnyika.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa kufutwa kwa mafao ya kujitoa msingi wake haupo kwenye marekebisho ya sheria yaliyofanyika Aprili13 mwaka huu pekee bali ni udhaifu katika mfumo mzima wa kisera na kisheria wa hifadhi ya jamii nchini, hali ambayo inahitaji wadau kutaka mabadiliko.
“Kufuatia kuanza kutumika kwa Sheria hiyo (ya 13 Aprili 2012) maombi mapya ya kujitoa yamesitishwa kwa kipindi cha miezi sita hadi pale miongozo itakapotolewa ili kuwezesha Mamlaka na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kutoa elimu kwa wadau

Mwananchi

Monday, October 15, 2012

Mnyika: Spika aunde Kamati ya Gesi


WAZIRI Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, amemtaka Spika wa Bunge, Anna Makinda, kutumia madaraka na mamlaka yake kutangaza kwa umma kamati nyingine ya kudumu ya Bunge itakayoshughulikia masuala ya gesi asili kabla na wakati wa mkutano wa Bunge ujao mwishoni mwa mwezi huu.
Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo kupitia CHADEMA, alisema hatua hiyo ni kutokana na hali tete na tata kuhusu sekta ndogo ya gesi asilia nchini na kwa kuzingatia umuhimu na unyeti wa sekta hiyo katika uchumi wa nchi na maisha ya wananchi.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Mnyika alisema pamoja na mambo mengine, Spika Makinda aelekeze kamati hiyo kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge ya mwaka 2011 kuhusu sekta ndogo ya gesi asili ikiwemo juu ya hatua iliyofikiwa katika kushughulikia tuhuma za ufisadi.
Madai mengine ni ya mapunjo ya fedha za mauzo ya gesi asili na hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya sera, mpango mkakati na sheria ya gesi asili.
“Hatua hii ni muhimu kufuatia ukimya wa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo kuhusu kauli yangu ya Oktoba 4, 2012 ya kutaka taarifa ya ufafanuzi kuhusu utafutaji wa mafuta na gesi asili nchini iliyotolewa na wizara hiyo Septemba 21 mwaka huu ifutwe,” alisema.
Alisema kuwa taarifa hiyo ya wizara ilieleza kuwa maandalizi ya sera ya gesi asili yapo katika hatua za mwisho wakati ambapo kamati mbalimbali za kudumu za Bunge hazijahusishwa katika mchakato huo muhimu pamoja na kuwa mamlaka ya kutunga sera kwa mfumo wa sasa ni ya Baraza la Mawaziri.
“Kwa unyeti na upekee wake sera ya gesi, Spika wa Bunge anapaswa kuwezesha Kamati za Kudumu za Bunge zihusishwe ili pawepo mashauriano na maridhiano kwa mapana na marefu,” alisema.
Mnyika alisema izingatiwe kwamba katika mkutano wa nane wa Bunge, Spika alitangaza kuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imevunjwa na kwamba majukumu iliyokuwa ikishughulikiwa yatashughulikiwa na kamati nyingine kwa mujibu wa madaraka na mamlaka ya spika.

Tanzania Daima

Sunday, October 14, 2012

KUMBUKUMBU YA BABA WA TAIFA MWALIMU JK NYERERE

Tukumbuke na kuuenzi wosia aliyotuachia  Baba wa Taifa Mwalimu Julias Kambarage Nyerere.

Saturday, October 13, 2012

Viongozi CHADEMA wanasurika kutekwa


VIONGOZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wamenusurika kutekwa baada ya gari lao aina ya Toyota Opa lenye namba za usajili T 850 BLK, kushambuliwa na watu wasiojulikana na kuvunjwa kioo cha nyuma na kitu kizito.
Tukio hilo lilitokea Oktoba 9, mwaka huu majira ya saa nne usiku wakati viongozi hao wakitoka katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani katika Kata ya Mpwapwa Mjini.
Shambulizi dhidi ya viongozi hao waliokuwa katika gari hilo mali ya Eva Mpagama ambaye ni Mratibu wa Vijana CHADEMA Mkoa wa Dodoma, lilifanyika katika eneo la Mwanakianga, nje kidogo ya mji wa Mpwapwa.
Walioshambuliwa ni Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo CHADEMA Taifa, Benson Kigaila, Mratibu wa Vijana Mkoa wa Dodoma, Mpagama na Kunti Yusufu ambaye ni mratibu wa akina mama CHADEMA mkoa.
Tukio hilo liliripotiwa Oktoba 10 katika kituo cha polisi cha Wilaya ya Mpwapwa, na kufunguliwa jalada namba RB/1934/2012.

Tanzania Daima

Friday, October 12, 2012

CHADEMA WAANZA MASHAMBULIZI SUMBAWANGA



CHADEMA kujadili ripoti za Mwangosi


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kuwa kinakusudia kufikisha ripoti za kamati mbalimbali zilizochunguza mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha television cha Chanel Ten katika kambi rasmi ya upinzani bungeni kwa ajili ya hatua zaidi.

Hata hivyo, mbali ya hatua hiyo, chama hicho kimesisitiza kuwa ni wakati muafaka kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emanuel Nchimbi, kuachia nafasi au awajibishwe na Rais Jakaya Kikwete, kutokana na kutumia fedha za wananchi kwa kamati waliyodai haikuwa na jipya juu ya mauaji ya Mwangosi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Waziri Kivuli wa Wizara hiyo, Vicent Nyerere, alisema wao kama chama wameona watoe tamko la awali wakati wakisubiri majumuisho ya pamoja kwa ajili ya hatua zaidi.

“Serikali toka awali haikuwa na nia ya kuonesha upungufu uliosababisha kifo cha Mwangosi, na kwa kutambua hili Nchimbi aliunda kamati yenye lengo la kuisafisha jeshi la Polisi kwa kutumia kodi zetu,”alisema.

Nyerere ambaye pia ni Mbunge wa Musoma Mjini, aliongeza kuwa ni jambo la ajabu kwa mtu kama Nchimbi kukubali kupokea ripoti ya ajabu na yenye kumdhalilisha kisha akasimama hadharani kuitetea.

Alisema ni wakati muafaka kwa Rais Kikwete kumfuta kazi Dk. Nchimbi kwa kuwa ameshindwa kujitathmini kutokana na mauaji yanayotokea sehemu mbalimbali hasa katika matukio ya kisiasa ili liwe fundisho kwa viongozi wengine katika kusimamia majukumu na maslahi ya Taifa.

Nyerere alibainisha kuwa namna kamati ya Dk. Nchimbi ilivyofanya kazi, imeshindwa kuwaelewesha watanzania kiini cha kifo hicho licha ya kutumia kodi zao, hivyo kushauri kuwa inapaswa kuundwa tume ya kimahakama.

Kuhusu maoni ya kamati ya Dk. Nchimbi juu ya shughuli za kisiasa kuishia bungeni baada ya uchaguzi, Nyerere alisema ni jambo la kushangaza kama leo Bunge litakuwa sehemu ya kunadi sera badala ya kuzungumzia matatizo ya wananchi.

“Kama kamati iliyo chini ya Jaji Ihema ndiyo imekuja na mtazamo huu wa kutaka shughuli za kisiasa na mijadala yake ifanyikie bungeni basi ninasisitiza kauli ya Tundu Lissu juu ya kumpinga Jaji huyu mstaafu ni muhimu zaidi,”aliongeza Nyerere.

Alisema ripoti ya kamati ya Nchimbi ingeweza kutoa taarifa zote hadharani bila kuingilia uhuru wa mahakama na kwamba alitaraji kuona ikiwagusa viongozi wa serikali moja kwa moja wanaoingilia shughuli za vyama vya siasa.

Kamati tatu tofauti zimetoa ripoti zake kuhusiana na mauji ya Mwangozi ambapo ile ya Baraza la Habari Tanzania na Jukwaa la Wahariri pamoja na ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, zimeeleza wazi kiini cha mauji hayo na kuwataja waliohusika.

Hata hivyo ripoti ya kamati iliyoundwa na Waziri Nchimbi ililalamikiwa kutokana na kushindwa kuweka taarifa kamili wazi kwa madai kuwa kesi ya mauaji hayo iko mahakamani.

Tanzania Daima

Thursday, October 11, 2012

Mbowe awaonya polisi


MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amelionya Jeshi la Polisi akisema haliwezi kuzima vuguvugu la mabadiliko (M4C) nchini kwa kutumia risasi kutisha na kuua wananchi.
Badala yake, amelitaka kufanya shughuli zake kwa utaalamu kwa kuzingatia sheria na kanuni zinazolisimamia na kuepuka kutumiwa kutekeleza matakwa ya watawala wanaowaagiza kuwanyanyasa wapinzani.
Mbowe alitoa onyo hilo juzi wakati akimnadi mgombea wa udiwani wa Kata ya Daraja mbili, Prosper Msofe katika Mtaa wa Jamhuri, ambaye hata hivyo hakuweza kuhudhuria mkutano huo kutokana na kulazwa Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru akipatiwa matibabu ya uti wa mgongo baada ya kushikiliwa na polisi.
Licha ya mgombea huyo kutokuwepo mkutanoni, Mbowe alimtaka kutotishika na tukio lililompata badala yake iwe changamoto ya kuzidi kudai na kupigania haki kwa maslahi ya umma.
“Kama sababu ya CHADEMA kuitwa chama cha vurugu ni kwa kutokana na hatua yetu ya kuwahamasisha watu kudai na kupigania haki zao, basi acha tuendelee kutambulika hivyo,” alisema.
Mbowe alieleza kushangazwa na hatua ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kushindwa kutangaza uchaguzi katika kata nne za Jiji la Arusha ambazo zilikuwa zinaongozwa na madiwani waliotimuliwa CHADEMA tangu mwaka jana licha ya juhudi walizofanya kuikumbusha kwa maandishi.
Kata hizo ni Elerai, Kimandolu, Kaloleni, Themi na Sombetini iliyokuwa ikishikiliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia aliyekuwa diwani wake, Alphonce Mawazo, ambaye alijivua gamba kwa kujiunga na CHADEMA.
“Woga wao wanajua nguvu ya CHADEMA kwa sasa, wanaogopa kuona tukishinda viti hivi na kuingiza madiwani sita pamoja na wa viti maalum, idadi ya madiwani wetu itakuwa kubwa, hivyo tutaongoza Halmashauri ya Jiji la Arusha,” alisema.
Akizungumzia utaratibu wa CHADEMA kuwachangisha wanachama wake fedha kwenye mikutano yao kwa ajili ya kuchangia gharama za uendeshaji, alisema kuwa chama kinajengwa na watu wenye fedha safi kama hizo.
Naye Mjumbe wa Baraza Kuu Taifa wa CHADEMA, Godbless Lema, aliwataka polisi wadogo kutokubali kutumiwa kutekeleza amri za kikandamizaji za viongozi wao kuumiza wananchi kwani mwisho wa siku watakaohukumiwa ni wao.
Alisema kuwa kwenye vurugu za Arusha za Januari 5 mwaka jana, walikufa watu watatu ambapo polisi wa vyeo vya juu ndio walioongezewa vyeo huku wale wa chini wakiambulia patupu.

Tanzania Daima

Wednesday, October 10, 2012

Mgombea udiwani CHADEMA alazwa


MGOMBEA udiwani kata ya Daraja Mbili kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA), Prosper Msofe, amelazwa kwenye hospitali ya mkoa ya Mount Meru akisumbuliwa na maumivu ya uti wa mgongo baada ya kuzuiliwa kwenye kituo cha polisi cha kati, Arusha usiku wa juzi kuamkia jana.
Katibu wa wilaya ya Arusha wa CHADEMA, Martin Sarungi, na aliyekuwa mbunge wa Arusha, Godbless Lema, waliwaeleza waandishi wa habari mbele ya kituo cha polisi kuwa mgombea wao alikamatwa majira ya saa mbili usiku eneo la Friends Corner baada ya kuhoji sababu wamachinga kunyang’anywa bidhaa zao na Ramadhan Kalamba (56) anayedai kuwa halmashauri ya jiji imempa jukumu la kuwaondoa machinga katikati ya jiji.
“Msofe alihoji sababu za Ramadhan kuchukua mali za wamachinga majira ya usiku wakati ambao halmashauri haifanyi kazi; alikuwa akizipeleka wapi na ni nani aliyempa mamlaka ya kuchukua vitu hivyo ndipo gari la polisi likafika na kumchukua,” alisema Lema.
Walisema kuwa baada ya kupata taarifa za mgombea wao huyo kukamatwa, baadhi ya wanachama na viongozi walimfuatilia mpaka kituo cha polisi kwa lengo la kumwekea dhamana jambo ambalo lilishindikana ndipo majira ya saa nne usiku wakaamua kuondoka.
Hata hivyo Kamanda wa Polisi mkoani hapa (RPC), Liberatus Sabas, alikanusha madai hayo kwa kile alichoeleza kuwa mgombea huyo hakunyimwa bali alikataa dhamana mwenyewe ambapo alidai kuwa alikamatwa na askari wa doria na kufikishwa polisi kwa tuhuma za kumpiga ngumi ya kifuani Kalamba.
Alisema kuwa jeshi la polisi lilipata taarifa kuwa Kalamba anashambuliwa ndipo askari wa doria walipofika na kumchukua Msofe ambapo alisema kuwa mzozo baina ya wawili hao ulitokana na hatua ya Msofe kuhoji sababu za Kalamba kutaka wamichinga hao waondoke eneo hilo huku akijaribu kumzuia asiendelee kutangaza.
Awali jana majira ya saa nne asubuhi mgombea huyo wa CHADEMA alienda kupatiwa matibabu kwenye zahanati ya polisi akiwa chini ya ulinzi mkali wa jeshi la polisi ambapo daktari wa zahanati hiyo alishauri apelekwe hospitali ya mkoa kwa uchunguzi zaidi lakini polisi waliamua kumpeleka mahakama ya mwanzo ya Maromboso.
Baadhi ya viongozi wa CHADEMA waliokuwa mahakamani hapo walikwenda kuuona uongozi wa mahakama na kuwaonyesha cheti alichopatiwa mtuhumiwa huyo kinachomtaka apelekwe hospitali ya mkoa kwa uchunguzi zaidi jambo ambalo linadaiwa pengine ndilo lililopelekea mtuhumiwa huyo kutofikishwa mbele ya hakimu.
Mgombea huyo ambaye alikuwa amepakiwa kwenye gari ya polisi yenye namba za usajili PT 1844 ambayo ubavuni imeandikwa OCD Arusha alikaa rumande ya mahakama hiyo kwa zaidi ya saa moja ambapo gari hilo lilirudi likiwa limeongeza idadi ya askari wenye silaha wakiongozwa na Mkuu wa Polisi wa wilaya hii (OCD), G. A Muroto na kumchukua ambapo walimpeleka moja kwa moja hospitali ya mkoa ya Mount Meru.
Wagombea wengine katika kinyang’anyiro hicho na vyama vyao kwenye mabano ni Philip Philip (CCM), Mohamed Msuya (NCCR-Mageuzi), William Laizer (TLP) na Zani Zakaria (CUF).

Tanzania Daima

Tuesday, October 9, 2012

Chadema yaibana Polisi kutoroka kwa watuhumiwa wa mauaji

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimelitaka Jeshi la Polisi kutoa maelezo ya kutosha yatakayoendana na uwajibikaji na hatua za kisheria, kufuatia watuhumiwa wawili wa mauaji ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama hicho, Kata ya Usa River, Msafiri Mbwambo, kutoroka mbele ya askari wenye silaha.

Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare, alisema chama hicho kimepokea kwa mshtuko kitendo cha watuhumiwa hao kutoroka mbele ya askari wenye silaha, baada ya kumnyang’anya bunduki mmoja wa askari waliokuwa lindo eneo la mahakama ya wilaya.

Alisema Chadema inasikitika kwa kitendo cha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, kugoma kutaja jina la askari aliyenyang’anywa bunduki na hata majina ya wenzake waliokuwa lindo mahakamani. 

Alisema kutokana na tukio hilo lenye utata, kuna umuhimu wa kuundwa kwa chombo huru cha uchunguzi wa mauaji yenye utata, yanayohusishwa na siasa, mojawapo likiwa ni tukio la mauaji ya Mbwambo.

Lwakatare alisema Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, katika barua aliyomwandikia Rais, alimtaka kuunda Tume ya Kijaji/ Kimahakama ya uchunguzi wa vifo vilivyotokea katika mikusanyiko, mikutano, maandamano au mazingira ya kisiasa yaliyohusisha Chadema.

“Ni bahati mbaya kuwa wakati Watanzania wapenda haki wakisubiri kujua majibu ya Rais kwa barua hiyo, masuala kadhaa yametokea, ambayo yote yameonesha kuwa serikali ya CCM inazidi kukomaza mfumo wa kulindana na kutaka kuficha masuala fulani fulani, hasa katika matendo ya mauaji yanayofanywa na Jeshi la Polisi,”alisema Lwakatare.


NIPASHE

CHADEMA waahidi makubwa


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani Mvomero, kimezindua kampeni ya udiwani wa Kata ya Mtibwa kwa ahadi mbalimbali ikiwemo kudai chenji ya fedha za mfuko wa jimbo kwa Naibu Waziri wa Utamaduni na Michezo na Mbunge wa jimbo hilo, Amos Makala, zinazodaiwa kutofanya kazi tangu mwaka 2010.
Uzinduzi huo uliofanyika kwenye uwanja wa Kambombe Madizini B, ulihudhuliwa na viongozi wa chama hicho kuanzia ngazi ya mkoa na wilaya za jirani, ulizinduliwa na Mwenyekiti wa Madiwani wa chama hicho mkoani hapa ambaye pia ni diwani wa Gairo, Dastan Mwendi.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Mwendi alisema: “Uoga na vitisho vya nguvu za dola ikiwemo kuua kwa makusudi raia nchini umetufikisha kwenye dimbwi la umasikini wa kutupwa tulio wengi na kuwanufaisha wachache walioko madarakani…wakati tunauawa na watoto kukosa elimu yenye tija inayotokana na kukosa huduma na vifaa wenzenu wananepa. Mchagueni Lucas Mwakambaya,” alisema huku akihoji zilipo fedha za jimbo tangu mwaka 2010”.
Akiwahimiza wapiga kura kumchagua Mwakambaya kuwa diwani wa Kata ya Mtibwa, Mwendi alisema muda wa Watanzania kugeuzwa ‘kuku wa kienyeji’ na kuwa wenye thamani wakati wa matatizo na furaha umepitwa na wakati kwa kuwa sasa wanaelewa haki zao.
Mwenyekiti wa chama hicho wa manispaa, Zuberi Kiloko na Mwenyekiti wa Vijana Mkoa, Boniface Ngonyani, waliungana na hoja hizo kwa nyakati tofauti na kusema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeelemewa na uongozi mbovu uliojaa rushwa na uonevu kwa wanachi.
“Chama makini huonekana hata katika uendeshaji wa michakato midogomidogo ya kichama, leo hii CCM inanuka rushwa hadi mwenyekiti wao Jakaya Kikwete amewashitukia na kutoa tamko kali kuwa atakayebainika kutoa rushwa atafutiwa uanachama, hii inatokana na kukithiri kwa rushwa,” alisema Kiloko.
Akijinadi mgombea udiwani wa Mtibwa, Mwakambaya, alitaja changamoto tisa zinazomkosesha usingizi na anazokusudia kuzifuatilia na kuzisimamia kikamilifu ikiwemo ya wenyeviti wa vijiji na vitongoji kutosoma taarifa za mapato na matumizi, upotevu wa sh milioni 28 kila mwezi na kutelekezwa kwa mnada miaka nane bila kuboreshwa huduma za kijamii.
Changamoto nyingine ni dhuluma zinazofanywa na kiwanda wa sukari cha Mtibwa ikiwemo ya kutolipa mafao ya wastaafu kwa miaka minane na fidia kwa waliohamishwa kupisha Sekondari ya Mtibwa, tatizo la ukosefu wa zahanati, soko, kuifuta michango isiyo na tija na kuikagua upya miradi yote iliyopo katani hapo.

Tanzania Daima

Mnyika: CCM ni janga


MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), amewataka Watanzania kukichukulia Chama cha Mapinduzi (CCM) na kukiona kama janga la kitaifa kwani kimeshindwa kutatua matatizo yao.
Kauli hiyo aliitoa juzi wakati wa uzinduzi wa kampeni ya uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata ya Msalato, manispaa ya Dodoma.
Mnyika alisena kuwa CCM imechangia kwa kiasi kikubwa kuwadidimiza Watanzania kutokana na kushindwa kusimamaia rasilimali zilizopo na kuwaruhusu wageni kuzitumia bila kuwashirikisha Watanzania.
Alisema kuwa Watanzania wengi wamekuwa maskini katika kipindi cha miaka 50 ya uhuru wakati kuna wachache ambao wanamiliki fedha nyingi.
CHADEMA wamemsimamisha Nsubi Bukuku kuwa mgombea udiwani katika kata hiyo.
Naye Afisa Habari wa CHADEMA, Tumaini Makene, alisema vurugu zilizotokea juzi kabla ya mkutano wao juzi zilisababishwa na wanachama wa CCM kuvamia msafara wao.
Majeruhi katika vurugu hizo ni Katibu wa UVCCM wa kata ya Kiwanja cha Ndege, Ali Swalehe; mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji wa CCM Dodoma Mjini, Fatma Mwihidini; Diwani wa kata ya Uhuru, Ali Kimaro; Hussein Mtengule na Waziri Shabani.
Hata hivyo, habari hizo zilisema kuwa hakuna mtu anayeshikiliwa na polisi kuhusiana tukio hilo hadi sasa.
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Stephen Zelothe, alipoulizwa kuhusiana na vurugu hizo alisema yuko safarini kurejea mjini Dodoma na kwamba angetoa taarifa kwa waandishi atakapofika.

Tanzania Daima

CHADEMA yazindua kampeni za udiwani


UMATI mkubwa wa watu, juzi ulijitokeza kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za mgombea udiwani wa kata ya Daraja Mbili wa Chama Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Prosper Msofe, uliofanyika kwenye mtaa wa Narvoi.
Aidha, viongozi wa chama hicho wakizungumza katika mkutano huo mbali ya kumuombea kura mgombea wao huyo, walitumia fursa hiyo kuutaka uongozi wa jiji la Arusha kuacha kufuata shinikizo la kisiasa katika kutafutia ufumbuzi suala la wafanyabiashara wadogowadogo maarufu kama machinga kwa madai kuwa suala hilo ni kama bomu la muda linalosubiri kulipuka.
Pia waliitaka serikali kutoa majibu yanayoeleweka juu ya tukio la kutoroka kwa washtakiwa wawili wa kesi ya mauaji ya aliyekuwa mwenyekiti wa CHADEMA, kata ya Usa River, Msafiri Mbwambo, kwa madai kuwa kuna uwezekano nyuma ya mpango huo, kukawa na mkono wa wanasiasa ambao hawataki ukweli ujulikane.
Mwenyekiti wa wilaya ya Arusha, Ephata Nanyaro alisema inashangaza kuona halmashauri ya jiji la Arusha inaamua kuendesha shughuli zake kijima kwa kuamua kugawa uwanja wa NMC.
Nanyaro ambaye pia ni diwani wa Levelosi, aliuataka uongozi wa jiji la Arusha kushughulikia masuala yote kitaalamu kuepuka kuibua migogoro isiyo ya lazima kama ilivyo sasa ambapo licha ya machinga kupewa eneo lisilotosheleza kwenye uwanja wa NMC, lakini idadi ya waliokosa ni kubwa hivyo badala ya tatizo kupungua limeendelea kuongezeka.
Kwa upande wake, aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, alisema serikali isifanyie mzaha suala la watuhumiwa hao kutoroka, kwani lina utata mkubwa na pia linaacha maswali mengi kuliko majibu.
Kampeni hizo zinatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 28, mwaka huu ambapo zinawashirikisha wagombea kutoka vyama vya CCM na TLP.

Tanzania Daima

CCM yaanguka tena


SASA UCHAGUZI MDOGO WANUKIA SUMBAWANGA
KWA mara nyingine tena, Chama cha Mapinduzi (CCM), kimegonga mwamba baada ya Mahakama ya Rufaa Tanzania, kuitupilia mbali rufaa ya aliyekuwa Mbunge wake wa Sumbawanga Mjini, Aeshi Hilaly, aliyevuliwa ubunge na Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga Aprili 30, mwaka huu.
Uamuzi wa kuitupilia mbali rufaa hiyo, umetolewa na jopo la majaji watatu, Januari Msoffe, Edward Rutakangwa na Engela Kileo, baada ya kubaini kasoro za kisheria.
Hilaly alivuliwa ubunge na aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Bethuel Mmila, kutokana na kesi iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea ubunge kupitia CHADEMA, Nobert Yamsebo.
Hata hivyo, Mei 28 mwaka huu, Hilaly alikata rufaa namba 55 ya mwaka 2012, dhidi ya Yamsebo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Justus Kalama na Vitus Kapufi, akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu.
Rufaa hiyo imebainika kuwa na dosari kadhaa ambazo zimeishawishi Mahakama ya Rufaa Tanzania chini ya jopo la majaji hao kuitupilia mbali jana katika uamuzi uliotolewa jijini Dar es Salaam.
Dosari hiyo ni kutokuwepo kwa mwenendo wa maombi ya mlalamikaji katika kesi ya msingi ya kuomba mahakama impangie kiwango cha fedha ambacho alipaswa kulipa kama amana ya kufungua kesi hiyo kwa mujibu wa Kifungu cha 111 (3) cha Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2010.
Katika uamuzi wake uliosomwa na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Zahra Maruma, mahakama hiyo ilirejea kifungu cha 111 (3) cha Sheria hiyo ya Uchaguzi.
Kwa mujibu wa kifungu hicho, Mahakama ilisema kwamba mtu anayefungua kesi ya uchaguzi, ni lazima awasilishe maombi ili mahakama impangie kiwango cha amana anachopaswa kulipa ndani ya siku 14 tangu kufungua kesi na kwamba ndani ya siku 14 nyingine tangu siku ya maombi hayo, mahakama hiyo iwe imeshapanga kiwango hicho.
Majaji hao waliongeza kuwa, ni muhimu kwa sababu kuu mbili, moja ni kuipa nafasi mahakama kuona kama maombi yaliwasilishwa ndani ya muda baada ya kesi kufunguliwa na pili kuona kama maombi hayo yaliamuliwa ndani ya muda tangu kuwasilishwa.
Kwamba kwa mujibu wa Kanuni ya 96 (1) na (3) za Kanuni za Mahakama ya Rufani, si jukumu la upande katika kesi kuamua kuwa nyaraka fulani ni muhimu au si muhimu katika rufaa, kama wakili wa Hilaly, Rweyongeza alivyodai.
Mbali ya kanuni hiyo, Mahakama hiyo pia ilirejea katika uamuzi wake katika rufaa namba 8 ya mwaka 2008, Fedha Fund Limited na wenzake wawili, dhdi ya George T.Varghese, pamoja na tafsiri ya Kanuni ya 85 (3) ya Kanuni za Mahakama ya Rufani ya Kenya za mwaka 1979.
"Kutokana na sababu hizo tulizokwisha kuzieleza hapo juu, tanarudia kusema kwamba kumbukumbu zinazohusiana na mwenendo wa maombi ya kupangiwa kiwango cha kulipa kama amana ni nyaraka muhimu katika rufaa.
Kutokuwepo kwa nyaraka hizo, rufaa haina nguvu chini ya Kanuni ya 96 (1) (k) ya Kanuni za Mahakama ya Rufani, hivyo rufaa inatupiliwa mbali," lilisema jopo hilo.
Hata hivyo, mahakama hiyo ilisema kuwa haiwezi kuamua upande wa warufani ulipe gharama za rufaa hiyo kwa kuwa kasoro zilizosababisha kutupiliwa mbali kwa rufaa hiyo ziliibuliwa na mahakama yenyewe.
Julai 3, 2012, AG na Kalama, nao walikata rufaa namba 65 ya mwaka 2012 dhidi ya Yamsebo wakipinga uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga.
Kutokana na rufaa hizo dhidi yake, Yamsebo kupitia kwa Wakili wake Victor Mkumbe, aliweka pingamizi la awali (PO) pamoja na mambo mengine akidai kuwa Hilaly hakuwa amelipia ada ya kufungua rufaa hiyo ya Sh 2000.
Hata hivyo, siku ambayo Mahakama ya Rufani ilipanga kusikiliza rufaa hiyo, iliamua kuziunganisha rufaa hizo mbili, ambapo Hilaly aliunganishwa na AG pamoja na Kalama wakawa waomba rufaa dhidi ya Yamsebo.
Kabla ya kuanza kusikiliza pingamizi la Yamsebo dhidi ya rufaa ya Hilaly, mahakama hiyo ilibaini kutokuwepo kwa mwenendo huo wa maombi ya Yamsebo kupangiwa gharama za kufungulia kesi hiyo ya msingi.
Kutokana na kasoro hiyo, mahakama ilihoji na kutaka maoni ya mawakili wa pande zote kuhusiana na kasoro hizo.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mwema Punzi alijibu kuwa wao walimwandikia barua Msajili wa Mahakama ya Rufani Kanda ya Sumbawanga kumuomba mwenendo wa kesi hiyo pamoja na vielelezo vingine na kwamba walipopewa, mwenendo wa maombi ya gharama za kesi haukuwemo.
Wakili wa Yamsebo, Mkumbe, alidai kuwa kutokana na kutokuwepo kwa mwenendo huo, kunaifanya rufaa hiyo iwe batili, na akaiomba mahkama hiyo iitupilie mbali.
Hata hivyo Wakili wa Hilaly, Richard Rweyongeza, alidai kuwa kukosekana kwa mwenendo huo hakuwezi kuifanya rufaa hiyo iwe ni batili, badala yake aliiomba mahakama hiyo itumie mamlaka yake chini ya Kanuni ya 2 ya Kanuni za Mahakama ya Rufani, ili iweze kuendelea.
Wakili Rweyongeza aliongeza kwamba hata ikibainika kuwa hizo gharama za kufunulia kesi hazikulipwa, anayeathirika ni mjibu rufaa, hoja ambayo iliungwa mkono na Wakili wa Serikali, Punzi.
Katika kesi hiyo ya msingi namba 01 ya mwaka 2010, Yamsebo alikuwa akipinga ushindi wa Hilaly, akidai kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa Katiba na Sheria ya Uchaguzi na hivyo kusababisha uchaguzi huo kutofanyika kwa haki na uhuru.
Pia, alikuwa akimtuhumu Hilaly na wafuasi wake kutoa rushwa kwa wapiga kura mbalimbali ili wamchague.
Tuhuma nyingine alikuwa akizieleka kwa Msimamizi wa Uchaguzi kuwa alibadilisha baadhi ya vituo vya kupigia kura kupelekwa mbali zaidi kati ya kilomita tano hadi nane, jambo ambalo ilichangia kuathiri matokeo ya uchaguzi huo.
Katika uamuzi wake, Mahakama Kuu ilikubaliana na baadhi ya hoja zilizotolewa na mlalamikaji na hatimaye kutengua ushindi wa Hilaly.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji Mfawidhi Betwell Mmila, alisema kuwa baada ya kupitia hoja zote, anashawishika kusema kuwa uchaguzi katika jimbo hilo ulikuwa si wa haki na huru.
Jaji Mmila alieleza kuridhika kuwa kulikwepo na mazingira ya rushwa na kutokuwapo kwa mazingira huru katika kampeni kwa baadhi ya maeneo.
Katika uchaguzi huo, Hilaly alitangazwa kuwa mshindi kwa kupata kura 17,328, huku Yamsebo akipata kura 17,132.
Kwa uamuzi huo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), itapaswa kuitisha upya uchaguzi ndani ya siku 90 ikiwa Hilaly hatakata tena rufaa kupinga uamuzi huo
wa jipo la majaji hao.

Tanzania Daima

Monday, October 8, 2012

CHADEMA yashinda rufaa Sumbawanga Mjini

Chama cha CHADEMA kimeshinda rufaa iliyokatwa na aliyekua mbunge wa SUMBAWANGA MJINI BW. AESH HILALY (CCM). Baada ya Rufaa hiyo kutupwa na hivyo kutoa fursa ya kufanyika kwa uchaguzi mdogo.

Habari kamili itawajia baadae.

Mlinzi wa Mbowe azua balaa CCM


MLINZI binafsi wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amezua balaa kubwa kwa Chama cha Mapinduzi mkoani Arusha kutokana na sura yake kufafanishwa na ile ya Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM) wilayani Arumeru, Boniface Mangaya Laizer, na hivyo kusimamishwa uongozi.
Laizer ambaye ni rafiki mkubwa wa kada wa CHADEMA mkoani Arusha, Ally Bananga, aliyejiengua CCM mapema mwaka huu, amedaiwa kuonekana kwenye picha gazetini akiwa na viongozi wa CHADEMA wakati wa operesheni ya chama hicho katika mikoa ya kusini hivi karibuni.
Akizungumza na gazeti hili jana kwa njia ya simu, Boniface alisema kuwa ameshangazwa na tuhuma hizo alizoziita kuwa ni mizengwe akidai kwamba hata huyo mlinzi wa Mbowe, Zakaria Swai, anayefafanishwa naye hamfahamu.
“Mimi sijawahi kuhudhuria mkutano wowote wa CHADEMA katika mikoa ya kusini na tuhuma hizo zilipoibuliwa nikalazimika kumtafuta huyo mlinzi ili nimfahamu. Katika picha iliyochapwa na gazeti moja la kila siku la Juni mosi mwaka huu, anaonekana Bananga akiwa na Mbowe na viongozi wengine na mlinzi huyo akiwa nyuma amevalia mawani meusi, sasa huyo watamfananishaje na mimi na kunisimamisha?” alisema.
Katika barua ya kujulishwa kusimamishwa kwake yenye kumb. Na. CM/AR/S/K. 13/3/Vol. V/233 ya Oktoba mosi, mwaka huu, ikiwa imeandikwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda, mwenyekiti huyo anajulishwa kuwa anasimamishwa kutokana na tuhuma za usaliti.
“ Tuhuma zinazokukabili za kiitikadi na usaliti ni nzito ambazo zinakuondolea sifa za kuwa kiongozi. Kamati ya siasa ya Halmashauri Kuu ya Mkoa iliyokutana kuanzia Septemba 27-29, mwaka huu, ilitafakari kwa kina tuhuma zinazokukabili na kwa Mamlaka iliyonayo kwa mujibu wa Katiba ya CCM ya 1977 Toleo la 2007- Ibara ya 96 (7) iliazimia kukusimamisha uongozi,” ilisomeka barua hiyo.
Chatanda katika barua hiyo anaongeza kuwa Boniface anajulishwa rasmi kwamba kuanzia sasa amesimamishwa uongozi hadi hapo mamlaka yenye uwezo juu yake ya kikatiba itakapoamua vinginevyo.
Hata hivyo, Boniface ambaye ameibuka na ushindi mkubwa katika uchaguzi uliomalizika hivi karibuni, alisema kuwa amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa UVCCM wilayani humo kwa taratibu zote za chama na hivyo akashangaa uamuzi huo umetoka wapi.
Alisema kuwa wapiga kura wake pia wameshangazwa na uamuzi huo aliodai kuwa ni mkakati wa viongozi wa mkoa kupandikiza kiongozi wanayemtaka wao awe mwenyekiti wa UVCCM wilayani Arumeru.
Naye rafiki yake wa karibu, Bananga, alizungumzia sakata hilo akisema huo ni ushuhuda tosha kuwa Chatanda baada ya kumaliza kutimiza azma yake ya kuvuruga vyama vya upinzani mkoani humo sasa dhambi hiyo imemrudia na kuanza kukibomoa chama chake.
“Mimi Boniface ni rafiki yangu wa karibu tangu nikiwa CCM hadi sasa, ila kutokana na CCM kutapatapa na makundi yao Arusha wanadhani ninamtumia kama pandikizi kuwabomoa. Anayeonekana kwenye ile picha si Boniface bali ni Swai mlinzi wa Mbowe,” alisema.
Bananga ambaye alikuwa Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Arusha na Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa kupitia mkoa huo, aliongeza kuwa Chatanda ni janga la kitaifa kwani amevuruga upinzani Arusha na sasa amegeukia chama chake.

Mwananchi

No comments:

Post a Comment