- Karismatiki ilianzishwa na Walokole
- Sasa Walokole hujichomeka katika Uamsho wa Kikatoliki
- ASKOFU: Chama cha kitume kinachodharau kingine marufuku
ASKOFU Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Mhashamu Methodius Kilaini na Mratibu wa Karismatiki Katoliki iliyopo Tanzania, Joseph Mshiri, wameweka wazi kuhusu kikundi cha Wanauamsho baada ya watu kutokielewa na kukitazama kama Ulokole ndani ya Ukatoliki.
Novatus Magege, muumini wa Parokia ya Kurasini, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, alipoulizwa anaijua vipi Karismatiki, alisema, “Hawa si ni Wanauamsho wa Kikatoliki.”
Kuhusu tofauti zao na Waprotestanti (Walokole), alisema.
“Tofauti yao ni kwamba Wanauamsho wanalitii Kanisa Katoliki na Walokole wao wana yao tu, hilo ndilo mimi ninafahamu.”
Bw. Joseph Magabe, wa Parokia ya Kiagata, Jimbo Katoliki la Musoma, yeye alipoulizwa kwa simu toka Musoma, alisema, “Kwa kweli hiyo Karismatiki mimi ninaisikia tu, sijui ni nini. Ila, nasikia wanafanya mambo kama Walokole. Sasa sijui vizuri labda wewe (mwandishi) unieleweshe vizuri.”
Mmoja wa waamini waliokuwa katika Mkutano wa Injili wa hivi karibuni uilofanyika katika Kanisa La Pentekoste Tanzania (KLPT), katika Parish ya Keko,jijini Dar es Salaam, alisikika akisema baada ya mkutano huo, “Mikutano ina faida bwana si unaona siku hizi hata Waromani (Wakatoliki) nao wanaifanya tunaona.”
Katika kutafuta ufafanuzi juu ya jambo hili linaloonekana kutoeleweka kwa jamii, kwa nyakati tofauti Gazeti la KIONGOZI lilikutana na Mratibu wa Karismatiki Bw. Mshiri.
Mshiri alisema, “… Wakarismatiki sio Walokole. Unajua wanaojiita Walokole sio dini wala dhehebu, hao ni watu wachache tu, wanaojiona kuwa wao ni cream yaani safi kabisa mbele ya Mungu kuliko watu wengine. Lakini, Wakarismatiki, kazi yao ni kutangaza Habari Njema.
Wana karama ya Kuhubiri Injili kwa kutumia zawadi (karama) za Roho Mtakatifu ambazo ndizo nyenzo maana Kristo anamuita kila mtu kumtumikia kwa karama yake na katika nafasi yake. Kama ni dereva aendeshe kama ni daktari, atibu watu.”
Akaongeza kuwa, “ Hawa wana karama ya kuhubiri na kuombea watu wengine hata wagonjwa.. .. hapa ni lazima kila mtu atambue ameitiwa nini katika kutumikia Ukristo.”
Kuhusu suala la kunena kwa lugha, Bw. Mshiri alikuwa na haya, ”Mtu anaanza mwenyewe kunena na wala sio kwamba anapata mafunzo mahali popote na ni vema hata Wakarismatiki wanajua wazi kuwa wakati mwingine, kunena kunaweza kuwakwaza watu wengine. Ndiyo maana hilo halifanyiki kanisani.”
Hata hivyo, anaongeza kuwa, “Kwa bahati mbaya ipo kasumba inayowanyemelea baadhi ya Wanakanisa kudhani kuwa Karismatiki ndiyo safi kuliko wengine na wengine wanapotoka kwa kudhani kuwa, kama mtu haneni kwa lugha, huyo eti hana Roho Mtakatifu. Hiyo si kweli. Hapo ndipo linakuja tatizo la watu wengine wenye karama kujiona wa juu kuliko watu wengine na hivyo, kuvunja umoja wa Kanisa.
Alisema kila Mkristo safi, hana budi kutodharau huduma ya mwingine.
Kuhusu kusali nje ya Kanisa, Bw. Mshiri alisema, “…Hatuwezi kuwafikia watu wengine wakiwamo Waislamu na wale wa madhehebu mengine kama hatutatoka nje ya kanisa kwa sababu, kanisani watu hawa hawaingii.”
Kuhusu suala hilo, yafuatayo ni maneno halisi ya Mhashamu Method Kilaini, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, juu ya Karismatiki Katoliki
“ILI kuelewa hili, kwanza tujue kwamba Kanisa Katoliki ni pana; na Mungu ni mpana ambaye kila wakati tunajifunza kitu kimoja na kingine kuona jinsi gani kinaweza kuleta msisimko. Katika mafundisho ya Kanisa yapo mambo mengi sana, na katika nyakati mbalimbali za kihistoria, mara unakuta kipengele fulani kameshikwa, kipengele kingine kimeingizwa sana.
Vyote hivi ni vipengele tofauti vya Kanisa hilo hilo ambalo linahamasisha Wakristo.
Unakuta wakati mwingine Moyo Mtakatifu wa Yesu, uliingia sana. Moyo Mtakatifu wa Mama maria ukaingia sana, Mtakatifu Anna na karama zake, ikaingia sana.
Katika kuelewa ukweli wa namna hiyo, tunaweza tukaelewa na Karismatiki.Kwanini Karismatiki inakuja leo; likuwa wapi na ilikuwa inafanya nini?
Karismatiki ni mojawapo ya vyama vya kitume ambavyo msisitizo wake unakuwa juu ya karama zake Roho Mtakatifu. Hii ina mwanzo wake kwani tangu mwanzoni mwa Kanisa, Wakristo wa mwanzo walisisitiza sana juu ya karama za Roho Mtakatifu.”
Anaendelea,”Kadri Kanisa lilipoanza liliweka mpango mmoja baada ya mwingine ili kuweka msisitizo wa karama ya kujitoa, kumbe misisimko ya haraka haraka ikapungua na kuwepo mipangilio ambayo inafanya vitu vilivyopangwa; kwamba tunaposali tufanye hivi, tufanye vile, hapa tuinue nikono, hapa tuiweke chini, ambapo sasa unaona katika Kanisa la mwanzo wakati wanafanya ule msisimko wa Roho Mtakatifu, ilikuwa ni ile hisia. Walitumia sana ile hali ya hisia.
Na kadiri muda ulivyokwenda hisia zilipungua na kukawepo na mipangilio ambayo inaeleweka. Lakini mara nyingine kuna uhitaji, hivyo katika kipindi tulichoingia na hasa baada ya Mtaguso wa Pili, ikatokea nafasi kwamba watu wenyewe vilevile waanze kuleta hisia zao katika namna wanavyofundisha na wanavyotoa msimamo wa dini.
Na katika hisia zao, zikaja karama zake Roho Mtakatifu ambazo ni kuhubiri; mtu akijisikia anahubiri, mtu anapoimba anaweza akaruka.
Zamani walikwambia hata mikono uifunge namna gani, na uifunge kwa kiasi gani.
Haya ni mambo ya kihistoria kwa sababu haya ni mambo ya binadamu anavyoitikia wito wa Mungu kufuatana na nyakati zake kufuatana na hali yake.
No comments:
Post a Comment