ALIYEPEPERUSHA BENDERA CHADEMA 2010 AREJEA KUTOKA MAREKANI, AUNGA MKONO Musa Juma na Moses Mashalla, Arusha WAKATI Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa akianza kugusa hisia za watu wanaomtaka agombee ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki, mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe amesema iwapo mtendaji mkuu huyo wa chama ataamua kuwania kiti hicho, wataheshimu uamuzi wake. Wakati Mbowe akitoa kauli hiyo, aliyepeperusha bendera ya Chadema katika uchaguzi wa mwaka 2010, Joshua Nasari na kutoa upinzani mkali kwa mgombea wa CCM, marehemu Jeremiah Sumari, naye amesema kama katibu mkuu wake ataamua kuwania kiti hicho, hatakuwa na pingamizi ikiwa chama kitaamua kwani lengo ni kutwaa jimbo hilo. Akizungumza na Mwananchi jana baada ya kuibuka mjadala kuhusu uwezekano wa Dk Slaa kuwania jimbo hilo, Mbowe alisema, "Katika suala la kugombea, utashi binafsi ni jambo la msingi...,kama Dk Slaa ataamua kugombea ubunge Arumeru Mashariki, tutaheshimu uamuzi wake." Mbowe alisema katika uteuzi wa chama, kuna vigezo vinavyoangaliwa ikiwa ni pamoja na jinsi mtu anavyokubalika kwa wananchi anakogombea, sifa zake na utashi wake binafsi na kuongeza, "Hatuna uteule katika chama." Hata hivyo, Mbowe alisema Chadema hakiwezi kumlazimisha Dk Slaa akagombee jimbo hilo kama mwenyewe utashi haumtumi kufanya hivyo, na kwamba hana shaka na kukubalika kwa katibu mkuu huyo kutokana na imani aliyojijengea kwa umma wa Watanzania. Mbowe alisema Dk Slaa amekuwa akiombwa kugombea ubunge katika maeneo mengi likiwamo Jimbo la Igunga, lakini chama kisingeweza kumlazimisha kwani jambo la kwanza ilibidi mwenyewe aonyeshe utashi binafsi wa kutaka kuwania kiti hicho. "Dk Slaa aliwahi kuombwa akagombee Igunga, lakini hakwenda. Hii ni kwasababu anakubalika nchini karibu kote, hivyo kama atakuwa na utashi binafsi kwanza, nadhani taratibu za chama zitatumika tu kufikia uamuzi," alifafanua. Mwenyekiti huyo wa Chadema pia alitoa angalizo kwamba, wakati mwingine uamuzi wa chama kupata mgombea unaangalia jinsi mgombea alivyo na mtandao katika jimbo analotaka kugombea ili hata kama akichaguliwa aonekane ni mbunge wa eneo hilo. "Ndiyo maana nasema kuna vigezo vingi tu, kwa mfano mtu anaweza kuwa mbunge mzuri bungeni, lakini je, ana connectivity (kinachomuunganisha) jimboni, kuangalia kama ana makazi na mtandao mwingine kwani asije akawa mbunge mzuri bungeni, lakini jimboni akiwa kama mgeni hivyo watu wakaona kama kimewapelekea pandikizi tu,"alifafanua Mbowe. Tangu juzi kumekuwa na mjadala katika mitandao ya kijamii huku baadhi wakimtaka Dk Slaa akagombee ubunge Arumeru Mashariki kuziba pengo la aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Marehebu Sumari, lakini wengine wanapinga na kumtaka aendelee kubaki na nafasi yake ya katibu mkuu wa chama kwa lengo la kukijenga. Hata hivyo, Dk Slaa ambaye katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 alishika nafasi ya pili akiwa nyuma ya Rais ya Jakaya Kikwete, juzi alinukuliwa na gazeti moja la kila siku (siyo Mwananchi) akisema, "Siwezi kulizungumzia jambo hilo, maana nilikwisha kusema muda mrefu kuwa sitaki tena ubunge na isitoshe mimi si mwenyeji wa Arumeru," Joshua Nasari Kwa upande wake Nasari (26) ambaye ana mtaji mkubwa wa kura kufuatia matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2010 alitoa msimamo wake akisema yupo tayari kufanya mazungumzo na viongozi wa juu ya chama chake juu ya kumpisha Dk Slaa kuwania ubunge katika jimbo hilo kama akihitaji. Nasari ambaye amerejea hivi karibuni mjini Arusha akitokea nchini Marekani, leo anatarajiwa kuchukua fomu rasmi ili kuwania nafasi hiyo kupitia Chadema. "Nimesikia maoni kupitia mitandao na wadau wakimuomba Dk Slaa kugombea, hili ni jambo jema kwetu kwani wananchi wanajua jimbo hili tunashinda Chadema na kama Dk (Slaa) akitaka kugombea dekomrasia ya chama chetu itafanya kazi, kwani kikubwa tunataka ushindi,"alisema Nasari. Nasari aliyewahi kuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso) kati ya 2008 na 2009 alipohitimu shahada ya Sayansi ya Jamii katika masuala ya utengenezaji Sera na Utawala, alisema ana imani Chadema kitashinda Arumeru. "Nilikuwa Marekani kikazi na sasa nimerejea kama ulivyoshuhudia watu wengi wananiunga mkono na tayari wamenichangia Sh 11milioni za kampeni na magari manane," alisema Nasari. Mgombea huyo ambaye tayari ametangaza kuacha kazi katika shirika la Kimarekani la Foundation For Tomorrow ili kujikita kwenye uchaguzi huo, alisema wakazi wa Arumeru Mashariki wanahitaji mwakilishi sahihi ambaye anaweza kuwatetea katika kuinua uchumi wao. Hata hivyo, alisema tayari amepata taarifa za Dk Slaa kutoa tamko kuwa hawezi kushiriki katika uchaguzi huo, kwa kuzingatia kuwa sio mkazi wa Meru na pia hana nia ya kugombea kiti hicho. "Nategemea Dk Slaa na viongozi wengine wa kitaifa, wakiwapo wabunge, marafiki zangu wa vyuo vikuu na wengine wengi tutakuwa nao Arumeru kuhakikisha Chadema inashinda,"alisema Nasari. Hadi kufikia jana, kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema Mkoa wa Arusha (Bavicha), Ephata Nanyaro, wanachama waliokuwa wamechukua fomu ni Yohane Kimuto, Samweli Chami na Rebecca Mwingisha na leo Nasari atakuwa mwanachama wa tatu. "Tunatarajia wanachadema wengi zaidi watajitokeza katika siku hizi zilizobaki ili kuchukuwa fomu na kurejesha mapema,"alisema Nanyaro. Mgombea CCM alalamikia rushwa Katika hatua nyingine, Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM katika Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Elirehema Kaaya ambaye pia ni afisa wa mifugo mkoani Mwanza, amekitaka chama hicho kukemea kampeni za fedha ndani ya chama katika uchaguzi huo. Kaaya ambaye pia aligombea jimbo hilo katika uchaguzi uliopita na kushindwa katika kura za maoni ndani ya CCM, alisema wakazi wa Arumeru hawahitaji mgombea wa CCM ambaye anapata nafasi hiyo kwa kutumia fedha. "Arumeru wanataka mtu wa kuwasemea matatizo yao mjengoni (bungeni) na sio mtu anayetumia fedha kupata ubunge na mimi naomba chama kikemee na kukomesha matumizi ya fedha,"alisema Kaaya. Akizungumzia maombi hayo, Katibu wa CCM Wilaya ya Arumeru Edson Lihweuli alionya mgombea yoyote ambaye atabainika kujihusisha na vitendo vya rushwa au kukiuka taratibu atachukuliwa hatua. Lihweuli alisema wagombea wote ambao wamechukua fomu, wamekuwa wakipewa taratibu hizo ili kuhakikisha uchaguzi ndani ya chama hicho unakwenda vizuri. Wakati huohuo, Mkuu wa shule ya Sekondari ya Leguruki inayomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Mwalimu Athony Msami jana alijitokeza kuchukua fomu na kufanya wagombea wa chama hicho wanaomba ridhaa ya chama kufikia sita.Wengine waliokuwa wamechukuwa fomu ni Sioi Sumari, mtoto wa aliyekuwa mbunge Jeremiah Sumari, William Ndeoya Sarakikya, Elipokea Urio, Elishiria Kaaya na Elirehema Kaaya. Wakati kada huyo wa CCM akichukua fomu, juzi jioni Mkurugenzi wa kituo cha Mikutano cha Arusha(AICC), Elishiria Kaaya alirejesha fomu na kueleza kuwa anagombea ili kutekeleza ilani kwa kushughulikia matatizo ya wananchi wa Meru. Kaaya ambaye pia aligombea uchaguzi uliopita na kuangushwa katika kura za maoni na Marehemu Sumari, alisema miongoni mwa mambo ambayo atayasimamia ni kuhakikisha anashirikiana na wananchi kukabiliana na matatizo ya upatikanaji maji, barabara, huduma za afya na masuala ya elimu. Takukuru yaanza kazi Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Arusha imekutana na wagombea waliojitokeza kuchukua fomu katika uchaguzi huo na kuwaonya kutojihusisha na rushwa pia kuwataka waheshimu sheria za gharama za uchaguzi. Takukuru pia imetamka kwamba tayari imeshashaanza kupokea malalamiko mbalimbali ya makada wa vyama tofauti vya siasa wilayani humo, kujihusisha na vitendo vya kutoa na kupokea rushwa na kwamba madai hayo yameanza kufanyiwa kazi. Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Takukuru mkoani Arusha, Mbengwa Kasumambuto imesema katika kujipanga kukabiliana na rushwa katika uchaguzi huo taasisi hiyo imekutana na wagombea wote wa vyama hivyo kwa lengo la kuwatahadharisha. “Katika kujipanga na uchaguzi wa Arumeru kwanza tumewaita wagombea ambao wameshajitokeza hadi sasa pamoja na viongozi wa vyama vyao, lengo ni kuwatahadharisha na kuwataka waheshimu sheria ya uchaguzi,”alisema Kasumambuto. |
Thursday, February 16, 2012
Mbowe: Dk Slaa ruksa kugombea Arumeru
Sunday, February 12, 2012
MATEMBEZI YA MSHIKAMANO Vs MAANDAMANO YA AMANI
Umati mkubwa sana wa wana CCM wakitembea kwa mshikamano juzi wakati wa maadhimisho ya miaka 35 ya kuzaliwa chama chao (hapa ni Iringa)
Umati wa wanaCHADEMA wakiwa kwenye maandamano yao mwaka jana (hapa ni Iringa)
Mwenyekiti nimeona niombe ufafanuzi wa mambo haya kwani naona kuna matumizi ya maneno tofauti kwa jambo lilelile kutokana na muhusika. inapokuwa CCM wanatembea pamoja wanasema ni matembezi ya mshikamano, bali wanapotembea CHADEMA huitwa maandamano.Sasa ni nini tofauti kati ya matembezi ya mshikamano na maandamano na kwa nini maandamano hupigwa marufuku wakati matembezi ya mshikamano hayazuiwi wala kukemewa kama maandamano? naamini uchambuzi na tafsiri zako mwenyekiti na nadhani utanipa tafsiri sahihi juu ya hili.asante
Tuesday, February 07, 2012
Uamsho ni Ulokole katika Ukatoliki?
- Karismatiki ilianzishwa na Walokole
- Sasa Walokole hujichomeka katika Uamsho wa Kikatoliki
- ASKOFU: Chama cha kitume kinachodharau kingine marufuku
ASKOFU Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Mhashamu Methodius Kilaini na Mratibu wa Karismatiki Katoliki iliyopo Tanzania, Joseph Mshiri, wameweka wazi kuhusu kikundi cha Wanauamsho baada ya watu kutokielewa na kukitazama kama Ulokole ndani ya Ukatoliki.
Novatus Magege, muumini wa Parokia ya Kurasini, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, alipoulizwa anaijua vipi Karismatiki, alisema, “Hawa si ni Wanauamsho wa Kikatoliki.”
Kuhusu tofauti zao na Waprotestanti (Walokole), alisema.
“Tofauti yao ni kwamba Wanauamsho wanalitii Kanisa Katoliki na Walokole wao wana yao tu, hilo ndilo mimi ninafahamu.”
Bw. Joseph Magabe, wa Parokia ya Kiagata, Jimbo Katoliki la Musoma, yeye alipoulizwa kwa simu toka Musoma, alisema, “Kwa kweli hiyo Karismatiki mimi ninaisikia tu, sijui ni nini. Ila, nasikia wanafanya mambo kama Walokole. Sasa sijui vizuri labda wewe (mwandishi) unieleweshe vizuri.”
Mmoja wa waamini waliokuwa katika Mkutano wa Injili wa hivi karibuni uilofanyika katika Kanisa La Pentekoste Tanzania (KLPT), katika Parish ya Keko,jijini Dar es Salaam, alisikika akisema baada ya mkutano huo, “Mikutano ina faida bwana si unaona siku hizi hata Waromani (Wakatoliki) nao wanaifanya tunaona.”
Katika kutafuta ufafanuzi juu ya jambo hili linaloonekana kutoeleweka kwa jamii, kwa nyakati tofauti Gazeti la KIONGOZI lilikutana na Mratibu wa Karismatiki Bw. Mshiri.
Mshiri alisema, “… Wakarismatiki sio Walokole. Unajua wanaojiita Walokole sio dini wala dhehebu, hao ni watu wachache tu, wanaojiona kuwa wao ni cream yaani safi kabisa mbele ya Mungu kuliko watu wengine. Lakini, Wakarismatiki, kazi yao ni kutangaza Habari Njema.
Wana karama ya Kuhubiri Injili kwa kutumia zawadi (karama) za Roho Mtakatifu ambazo ndizo nyenzo maana Kristo anamuita kila mtu kumtumikia kwa karama yake na katika nafasi yake. Kama ni dereva aendeshe kama ni daktari, atibu watu.”
Akaongeza kuwa, “ Hawa wana karama ya kuhubiri na kuombea watu wengine hata wagonjwa.. .. hapa ni lazima kila mtu atambue ameitiwa nini katika kutumikia Ukristo.”
Kuhusu suala la kunena kwa lugha, Bw. Mshiri alikuwa na haya, ”Mtu anaanza mwenyewe kunena na wala sio kwamba anapata mafunzo mahali popote na ni vema hata Wakarismatiki wanajua wazi kuwa wakati mwingine, kunena kunaweza kuwakwaza watu wengine. Ndiyo maana hilo halifanyiki kanisani.”
Hata hivyo, anaongeza kuwa, “Kwa bahati mbaya ipo kasumba inayowanyemelea baadhi ya Wanakanisa kudhani kuwa Karismatiki ndiyo safi kuliko wengine na wengine wanapotoka kwa kudhani kuwa, kama mtu haneni kwa lugha, huyo eti hana Roho Mtakatifu. Hiyo si kweli. Hapo ndipo linakuja tatizo la watu wengine wenye karama kujiona wa juu kuliko watu wengine na hivyo, kuvunja umoja wa Kanisa.
Alisema kila Mkristo safi, hana budi kutodharau huduma ya mwingine.
Kuhusu kusali nje ya Kanisa, Bw. Mshiri alisema, “…Hatuwezi kuwafikia watu wengine wakiwamo Waislamu na wale wa madhehebu mengine kama hatutatoka nje ya kanisa kwa sababu, kanisani watu hawa hawaingii.”
Kuhusu suala hilo, yafuatayo ni maneno halisi ya Mhashamu Method Kilaini, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, juu ya Karismatiki Katoliki
“ILI kuelewa hili, kwanza tujue kwamba Kanisa Katoliki ni pana; na Mungu ni mpana ambaye kila wakati tunajifunza kitu kimoja na kingine kuona jinsi gani kinaweza kuleta msisimko. Katika mafundisho ya Kanisa yapo mambo mengi sana, na katika nyakati mbalimbali za kihistoria, mara unakuta kipengele fulani kameshikwa, kipengele kingine kimeingizwa sana.
Vyote hivi ni vipengele tofauti vya Kanisa hilo hilo ambalo linahamasisha Wakristo.
Unakuta wakati mwingine Moyo Mtakatifu wa Yesu, uliingia sana. Moyo Mtakatifu wa Mama maria ukaingia sana, Mtakatifu Anna na karama zake, ikaingia sana.
Katika kuelewa ukweli wa namna hiyo, tunaweza tukaelewa na Karismatiki.Kwanini Karismatiki inakuja leo; likuwa wapi na ilikuwa inafanya nini?
Karismatiki ni mojawapo ya vyama vya kitume ambavyo msisitizo wake unakuwa juu ya karama zake Roho Mtakatifu. Hii ina mwanzo wake kwani tangu mwanzoni mwa Kanisa, Wakristo wa mwanzo walisisitiza sana juu ya karama za Roho Mtakatifu.”
Anaendelea,”Kadri Kanisa lilipoanza liliweka mpango mmoja baada ya mwingine ili kuweka msisitizo wa karama ya kujitoa, kumbe misisimko ya haraka haraka ikapungua na kuwepo mipangilio ambayo inafanya vitu vilivyopangwa; kwamba tunaposali tufanye hivi, tufanye vile, hapa tuinue nikono, hapa tuiweke chini, ambapo sasa unaona katika Kanisa la mwanzo wakati wanafanya ule msisimko wa Roho Mtakatifu, ilikuwa ni ile hisia. Walitumia sana ile hali ya hisia.
Na kadiri muda ulivyokwenda hisia zilipungua na kukawepo na mipangilio ambayo inaeleweka. Lakini mara nyingine kuna uhitaji, hivyo katika kipindi tulichoingia na hasa baada ya Mtaguso wa Pili, ikatokea nafasi kwamba watu wenyewe vilevile waanze kuleta hisia zao katika namna wanavyofundisha na wanavyotoa msimamo wa dini.
Na katika hisia zao, zikaja karama zake Roho Mtakatifu ambazo ni kuhubiri; mtu akijisikia anahubiri, mtu anapoimba anaweza akaruka.
Zamani walikwambia hata mikono uifunge namna gani, na uifunge kwa kiasi gani.
Haya ni mambo ya kihistoria kwa sababu haya ni mambo ya binadamu anavyoitikia wito wa Mungu kufuatana na nyakati zake kufuatana na hali yake.
Sumry Hii!
Taswira Kutoka Bungeni Mjini Dodoma
Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja akijibu maswali ya wabunge kuhusu upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini na uondoaji wa tatizo la mgawo wa umeme unaoendelea kwenye baadhi ya maeneo nchini na kufafanua kuwa serikali inaendelea na mikakati ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya utoaji wa huduma ya umeme katika maeneo yasiyo na huduma hiyo na kuimarisha uzalishaji wa umeme wa uhakika katika Gridi ya Taifa kupitia vyanzo mbalimbali.
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR –Mageuzi) David Kafulila akichangia bungen kuhusu namna bora ya ukusanyaji wa mapato kupitia kodi zinazotozwa kwenye makampuni ya simu nchini ili kuongeza mapato ya serikali leo mjini Dodoma.
Waziri na Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hadji Mponda(kushoto) akizungumza jambo na Waziri Mkuu Mizengo Pinda (kulia)ndani ya ukumbi wa Bunge leo mjini Dodoma.
Naibu spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugay akitoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali zilizowasilishwa na wabunge wakati wa kikao cha tano cha mkutano wa sita leo mjini Dodoma.
Naibu Waziri Wa Viwanda na Biashara Lazaro Nyalandu,Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe na Ezekiel Wenje(CHADEMA)Watembelea Ubalozi wa Tanzania Nchini Marekani
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mh. Lazaro Nyalandu akisaini kitabu cha wageni.
Kiongozi kambi ya Upinzani Bungeni, Mh. Freeman Mbowe akisani kitabu cha wageni.
Waziri kivuli wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kiamtaifa, Mh. Ezekia Wenji akitia saini kitabu cha wageni.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara wa Tanzania, Mh. Lazaro Nyalandu (kulia) akiwa pamoja na Waziri kivuli Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Ezekia Wenje wakiwa kwenye mkutano na Maofisa wa Ubalozi wa Tanzania Nchini Marekani, Ijumaa February 3, 2012 katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania, Washington, DC.
Kushoto ni Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mh. Lazaro Nyalandu akiwa na Kiongozi wa kambi ya Upinzani Bungeni, Mh. Freeman Mbowe (CHADEMA).
Thursday, February 02, 2012
Subscribe to:
Posts (Atom)